Pages

Subscribe:

Monday, 15 February 2016

UTAMU WA NENO LA MUNGU

BIBLIA NI NENO LA MUNGU LILILO HAI Katika Biblia Yako Soma Zaburi 119: 9-11,105; Waebrania 4:12; Marko 4:21-29. Mstari Wa Kukariri Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema (2Tim 3:16, 17). Baadaye Zungumzieni Jambo Hili Je, unaamini kuwa Neno la Mungu ndilo lenye mamlaka yote katika maisha? Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena Jitahidi kutenga muda maalum kila siku kwa ajili ya kutulia na kutafakari. Tekeleza mpango wa kusoma Biblia. Andaa alama saba za kuweka katika Biblia yako pale unapoachia kusoma ili uweze kupapata kirahisi utakapoendelea kupasoma tena wiki inayofuata. Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada Kutoka katika 2Fal 22:8-13 na 2Fal 23:1-32 andika mageuzi yote aliyoyafanya mfalme Yosia baada ya kulisikia neno la Mungu. Tafakari Andiko Hili Mathayo 7:24-27 Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu Ombea taifa la Ujerumani. Idadi ya watu: 80,000,000. Idadi ya Wakristo ni 75% Ujerumani Mashariki maskini na Ujerumani Magharibi tajiri sasa zimeungana. Makanisa ya zamani yanapoteza watu. Uamsho unatakiwa haraka 1. Biblia Ni Neno La Mungu Kwa kila mwamini neno la Mungu ni la kipekee na la thamani kubwa. Kwa karne nyingi zilizopita watu wengi wametoa maisha yao katika kuhifadhi kweli ya neno la Mungu kwa ajili yetu ili tupate kusoma. Kwa kuzingatia thamani kubwa ya neno la Mungu, na andiko kutoka Mk 4:21, swali ni hili, ‘Biblia iko wapi katika maisha yako?’ Je, imefichwa mbali; Au imewekwa mahali pa juu ili ipate kumulika kila eneo la maisha yako? 2. Baraka Katika Neno La Mungu Neno lake li hai, linanena nawe na kutenda kazi ndani yako (Ebr 4:12,13). Neno lake ni kioo kinachokufanya ujione ulivyo kadiri unavyoendelea kulisoma. Neno lake kamwe halitakufanya ujidanganye mwenyewe, wala kuficha ukweli (Yak 1:22-24) (Mk 4:22). Neno lake litakuandaa kikamilifu ili uwe, na ufanye kile Mungu anachotaka (2 Tim 3:15-17). Kuanzia ulipokuwa mtoto hadi sasa umeyajua Maandiko Matakatifu yanayoweza kukupa hekima unayoihitaji kwa ajili ya kupata wokovu kwa imani katika Kristo Yesu. Maandiko yote yana pumzi ya Mungu na yanafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema. Inasemekana, na ndivyo ilivyo, kwamba Biblia ni Mwana wa Mungu katika maandishi, kwa sababu Yesu anaitwa ni Neno, na vilevile anaitwa Kweli (Yn 1:1). Je, Unataka Kufanikiwa Na Kustawi? Basi fanya yale Yoshua aliyoagizwa kufanya (Yos 1:8). Na kama unataka kustawi kwa kila kitu zingatia Zab 1:1-3. 3. Je, Unaposoma Unasikia? Je, umewahi kugundua kuwa unaposoma neno la Mungu ‘unasikia’ kwa ndani na si kwa masikio ya nje? Hiyo ni sauti ya Mungu. Yapasa tuwe makini na kile tunachosikia kwa sababu kwa kipimo kilekile tunachotumia, ndicho tutakachopimiwa (Mk 4:24). 4. Je, Unalitumiaje Neno La Mungu? Unalitumia hilo neno kufanya upya moyo wako (Rum 10:17). Unalitumia hilo neno kufanya upya mawazo yako Rum 12:2). Unalitumia hilo neno kufanya upya maneno yako (Rum 10:10) (Mit 18:2). Ulitumie hilo neno kufanya upya matendo yako (Yn 14:15). Ulitumie hilo neno kuimarisha ushindi wako. Shetani hakuwa na usemi Yesu aliposema, ‘Imeandikwa’! (Mt 4:1-11)-zingatia mistari ya 4,7 na 10. Litumie Neno Kuhuisha Maombi Yako Waamini wa kwanza mara kwa mara walinukuu maandiko ili yawaongoze katika maombi, na Mungu alijibu haraka (Mdo 4:23-31). Iwapo utaomba kwa kutumia neno la Mungu, yafuatayo yataanza kutokea: Kwanza, unapanda mbegu ya neno. Kisha kwa uvumilivu katika kuliomba neno, na saburi, huja masuke. Na kwa kadiri unavyoendelea kuwa na imani kwa Mungu na katika neno lake, huja ngano pevu, nafaka kukomaa na hatimaye mavuno. (Mk 4:14, 26-29) (Isa 55:10, 11) (Mwa 8:22). Ni Muhimu Kuwapa Wengine Neno La Mungu Ni muhimu kwa sababu ye yote mwenye neno la Mungu anaweza kuokolewa na kupewa zaidi, mathalani: uponyaji, uhuru, uongozi, baraka na ustawi, kwa kuliamini. Lakini mtu asiye na hilo neno la Mungu ili kuliamini na kulifanyia kazi, hana baraka yo yote katika hizo zilizotajwa, na atapoteza hata hicho alichonacho, yaani maisha yake na nafsi yake milele (Mk 4:25). 5. Unapataje Kulisikia Neno? Mungu amefanya iwe rahisi sana kuisikia sauti yake. Wewe kaa peke yako na Yeye, na kisha fungua Biblia yako. Kiri udhaifu wako na omba kujifunza kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Chukua muda kutafakari yale uliyosoma na kusikia, kwa sababu kwa njia hiyo utashangaa kuona jinsi Mungu atakavyozungumza na wewe na kujibu maswali yako. Nikiwa mwamini mpya sikuyajua mambo haya. Nilihudhuria kwenye kusanyiko la maombi na kimyakimya niliomba kwa ajili ya kazi yangu, nikamwombea mke wangu na watoto kwa sababu ya matatizo yote tuliyokuwa nayo. Baada ya muda mfupi nilihisi msukumo wa kuichukua Biblia yangu na ikafunguka yenyewe katika Zaburi ya 128. Na nilipoanza kusoma Mungu alinistusha na baadaye akanipooza kwa neno lake akiuambia moyo wangu: “Wamebarikiwa wote wamchao Bwana na kutembea katika njia zake. Utakula matunda ya kazi yako, baraka na kustawi vitakuwa vyako. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, na wanao kama matawi ya mtende mezani pako”. Naliliamini neno la Mungu na leo hii, baada ya miaka kadhaa kupita naweza kuona jinsi Mungu alivyoitunza ahadi yake kwa kuibariki familia yangu na kazi yangu. 6. Namna Ya Kufurahia Usomaji Wa Biblia Watu wengi huanza na kitabu cha Mwanzo na baadaye huacha wanapokutana na sehemu ngumu katika Agano la Kale ambazo hawazielewi. Sisi sote tunapenda kula vyakula mbalimbali siku kwa siku, na hivyo ndivyo ilivyo hata kwa chakula cha kiroho. Jaribu kufuata mpangilio ufuatao nawe utapata mlo tofauti kila siku. Kila siku soma Zaburi za kuabudu na Mithali kwa ajili ya kupata hekima.

0 comments:

Post a Comment