Pages

Subscribe:

Monday, 3 April 2017

TOA SADAKA INAYOMGUSA MUNGU


“Utoaji ulio mwema ni mlango wa mafanikio na uponyaji wa kimwili, kiuchumi,
na kiroho” Dhabihu igusayo moyo wa Mungu
ni mlango wa baraka yako.

Watu wengi wamekuwa wakitamani sana kubarikiwa na Mungu ila si wepesi kutaka
kujua ni kwa namna gani au zipi ni kanuni za Mungu kwa mafanikio yao.

Wengine kwa kutojua utaratibu wa Mungu wameamua hata kuvutwa na makanisa
yanayotangaza kuwa wana ibada za kuombea watu Baraka na utajiri,

ila Mungu yeye ni wa utaratibu na ukimgusa katika maeneo yake aliyoamuru yafanywe ni lazima utabarikiwa
hata pasipo kuombewa na mitume na manabii,

Ni muhimu sana kwa kila mtu kujifunza njia za Mungu na kujua ni kwa namna gani
Mungu anawabarika watu wake.

Nyakati za leo ni rahisi sana kukuta mtu anamdai
Mungu mambo mengi na Baraka ila ukitazama maisha yake jinsi yalivyo hakuna
utoaji na si mwepesi kufanya mambo yanayobariki moyo wa Mungu.

Vipo vitu vinavyougusa moyo wa Mungu moja kwa moja,
na vipo vitu vinafanyika na vimebeba sura nzuri ila si vyote vinavyougusa moyo wa Mungu.

Katika sadaka kuna sadaka inayougusa moyo wa Mungu moja kwa moja na kuna
dhabihu itolewayo katika madhabahu ya Mungu ila haina sifa ya kugusa moyo wa Mungu.

Maandiko matakatifu yanatueleza kuwa utoaji ulio wa moyoni pasipo kushinikizwa
ni sababu ya watu kubarikiwa na pia kukosa roho ya utoaji ubaki kuwa sababu ya watu kutobarikiwa.

       Marko 5:30-32
“Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka
kati ya mkutano,
akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu?

Wanafunzi wake wakamwambia,
je!
Wawaona makutano wanavyokusonga-songa, na wewe wasema ni nani aliyenigusa?”

Watu wengine waliokuwa katika eneo lile walimpapasa Yesu ila hakuona mguso wowote,

tofauti ni kwa Yule mama ambaye aligusa kwa mguso wa kudhamilia ambao uligusa moyo wa Mungu moja kwa
moja na ukamfanya Mungu aingilie kati suala la Yule mama na kumponya.

Si kila agusaye ana mguso wa kugusa moja kwa moja,
kuna wengine wanapapasa tu ila hawagusi ila kuna wengine wanagusa kabisa
mpaka wanatoa mshituko na muitikio wa tofauti kwa mguswaji,

mpapasaji hana athari yoyote ile ila mgusaji anaathari kubwa sana,

na mgusaji aweza patiwa mambo mengi sana kwa kule tu kugusa kwake.

         Marko 12:44-44
“Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina,
akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku.

Matajiri wengi wakatia mengi.

42 Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini,
akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa.

43 Akawaita wanafunzi wake, akawaambia,
Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina;

44 maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi;
bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.”

Suala si kutoa ila suala ni kutoa dhabihu igusayo moyo wa Mungu kwa moja kwa moja,
mtu unayeweza kumpima kwa viwango vyako vya kawaida kuwa yuko chini sana ndiye anaweza kuwa mtu afanyaye mambo
yanayougusa moyo wa Mungu na kumfanya ajisikie vizuri.

Aidha katika eneo la sadaka kuna watu wengi watatoa dhabihu zao kama wapapasaji,
ila kuna mmoja atatoa dhabihu ambayo itaugusa moyo wa Mungu moja kwa moja
na kumfanya Mungu asiwe na kimya na ashuke na kusababisha uponyaji wa maeneo yote kwa huyo mtu.

Dhabihu itolewayo kwa moyo na kupenda mbele za Mungu uwa inasema na
kumkumbusha Mungu mara zote kwa habari yetu na maisha yetu.

Ni kweli kuwa maombi tuyaombayo uzungumza
sana mbele za Mungu, ila dhabihu tuzitoazo kwa moyo zinapaza sauti njema sana mara zote mbele za Mungu huku zikimkumbusha
Mungu kuwa imempasa hatubariki.

Kweli kuna wakati aweza kaa kimya kabisa
ila akitazama moyo wako wa kumtolea na kujitoa mbele zako ni lazima aitike na kufanya
hata zaidi ya yale uyaombayo.

Maandiko usema yeye ufanya zaidi ya yale tuyaombayo,
ushawahi kujihoji ndani yako kuwa ni nini
kinamshawishi afanye zaidi ya yale tuyatamkayo katika kuomba kwetu?

Ni kweli kuwa kuna neema ila pia dhabihu uzitoazo zinadai ulinzi, uponyaji, utajiri na mali,
na heshima mbele za Mungu kwa maisha yako.

Mfano Kornelio sadaka alizokuwa akitoa kuwasaidia watu wengi wenye shida zilifika
mbele za Mungu na kumkumbusha Mungu kuwa inapaswa afanye jambo kwa mtu wake Kornelio.

      Mwanzo 4:3-5
“Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA.
4 Habili naye akaleta
wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama, BWANA akamtakabali
Habili na sadaka yake;

5 bali Kaini hakumtakabali wala sadaka yake, Kaini akagadhabika sana, uso wake ukakunjamana.”

Suala si kutoa tu ila suala ni kutoa dhabihu yenye kupendeza mbele za Mungu.

Kaini alikuwa anatoa tena sana ila tatizo alikuwa anatoa ziada za vile alivyonavyo na tena
si vile vizuri,
nadhani hakufahamu kuwa,
“kipimo kile kile upimacho ndicho utapimiwa”.

Tofauti kwa Habili ni ya kuwa yeye alitoa kila kilicho bora mbele za Mungu, kile
ambacho ni kizuri na chenye kupendeza ndicho alichochagua kumpa BWANA, maandiko
yanaeleza kuwa Mungu aliikubali na kuipokea sadaka ya Habili na akaikataa sadaka ya Kaini.

Kama si mtoaji au unatoa sadaka mbovu usijadili sana kwa nini mambo yako hayako vizuri.

Jawabu unalo kuwa Mungu anakubali sana sadaka itolewayo kwa moyo na yenye kupendeza.

Ni dhahiri kuwa kukosa roho ya utoaji na kuwa na tabia ya kumkadiria Mungu katika yale tuyatoayo ni sababu kubwa sana
ya kutopokea baraka za Mungu.

Watu wengi sana huwa na tabia njema ya kupenda kutoa kama ilivyokuwa kwa Kaini na Habili,

ila katika kupenda huko wengi hutoa ziada ya vile walivyonavyo na wakati mwingine
uchagua vitu ambavyo wanaona kwao vimepoteza thamani na ndivyo uvitoa kwa wengine.

Kutoa ziada ya vitu ulivyonavyo na kuchagua kibovu katika vizuri kamwe hakuwezi
kugusa moyo wa Mungu hata akageuka kama alivyogeuka kwa mama Yule aliyemgusa.

Wengine usema kuwa mimi ninatoa sana ila naona kama sibarikiwi,
jiulize kama unatoa kwa namna njema inayoweza
kumgusa moyo wa Mungu.

Nakumbuka siku moja nikiwa nimesafiri kuelekea mahali pa faragha kwa ajili ya maombi binafsi,

nikiwa huko nilipata mguso wa tofauti sana wa kutoa mavazi yote ya thamani niliyokuwa
nayo nimpatie mtu wa Mungu ambaye nilimkuta katika eneo hilo, suala hili lilikuwa gumu sana,

haswa ukizingatia nami sikuwa na mavazi mazuri na ya kupendeza zaidi ya yale,
nilishindana na ile sauti ya kufanya jambo hili,

ila mwisho nikaona ni vyema niitii ile sauti na kutoa,
haikuchukua muda mrefu kuna mama mmoja alikuja nyumbani na kuleta nguo nyingi zaidi ya zile nilizotoa na kupata viatu vizuri,

kwangu hii ni uaminifu wa Mungu asemaye, “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa;

kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu
watakachowapa kifuani mwenu.

Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakacho pimiwa”

Dhabihu inayougusa moyo wa Mungu ni dhabihu inayouma katika moyo wa mwanadamu,
yaani kutoa kitu ukipendacho na ukionacho
kuwa bora kuliko vyote na wapenda kukitumia

ila kwa ajili ya BWANA unaamua kutoa si jambo rahisi na kufanya hivyo ni ishara ya upendo sana kwa Mungu na huonyesha
kuwa unamjua unayemtumikia.

Yaani dhabihu ambayo yaweza kuugusa moyo wa Mungu hata wewe mwenyewe ukitoa unaona umetoa kitu mbele za BWANA
na wakati mwingine hata nafsi yako yagoma kabisa kwa kuwa nafsi ina tabia ya kujipenda yenyewe.

        Mwanzo 22:2
“Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee,
umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria,
ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”

Mungu anamtaka Ibrahimu atoe mtoto pekee aliye naye na ampendaye, si jambo rahisi kwa watu walio wengi kufanya hivi.

Kwa mfano huu ni sawa na umeangaika kupanga miaka mingi sana halafu unapata tu nyumba yako mwenyewe ukasikia
Mungu anakuambia nataka utoe hiyo nyumba uliyonayo umpatie mtu Fulani, au umetembea

muda mrefu sana kwa miguu halafu umepata gari zuri la pekee na ulipendalo sana

halafu ukasikia Mungu anakuambia toa hilo gari umpatie mtu Fulani si jambo rahisi kabisa.

Lakini toa, heri kutii na kukubali, utauona mkono wa Mungu kwako.

Asante kwa kufuatana nami, zaidi endelea kuitembelea blog hii.

Ni mimi rafiki na ndugu yako mpenzi

        Ev. Elimeleck S Ndashikiwe

          +255767445846 &
          +255715445846.

3 comments:

  1. Amen nimelipenda somo hili sana

    ReplyDelete
  2. Nimepata kitu mhimu ila inahitaji uushinde mwili kwenye hili ili roho ipate kupona

    ReplyDelete