Pages

Subscribe:

Wednesday, 10 February 2016

UCHAMBUZI YOHANA 17:11-26

Sura ya 17 ya Kitabu cha YOHANA, kwa kutafakari YOHANA 17:11-26.

Ingawa kichwa cha somo letu la leo ni, “UMOJA ALIOTUOMBEA YESU“,

kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.
Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele kumi na viwili:-

(1) MAOMBI YA UMUHIMU WA KWANZA (MST. 11-24);
(2 KUTOA HOJA ZENYE NGUVU KATIKA MAOMBI (MST. 11-24);
(3) UWALINDE HAWA (MST. 11-12); (4) WAJIBUWA KUWATUNZA WATOTO WACHANGA KIROHO (MST. 12);
(5) UMOJA ALIOUTUOMBEA YESU (MST. 11, 21-23);
(6) KUWA NA FURAHA YA YESU ILIYOTIMIZWA NDANI YETU (MST. 13);
(7) KUCHUKIWA KWA MTU ANAYELIPOKEA NENO (MST. 14); (8) SIOMBI UWATOE KATIKA ULIMWENGU (MST. 15);
(9) WAO SI WA ULIMWENGU (MST. 16);
(10) UWATAKASE (MST. 17, 19); (11) KAMA ULIVYONITUMA NAMI NALIWATUMA (MST. 18);
(12) YATUPASAYO KUFANYA BAADA YA KUMJUA MUNGU (MST. 25-26).

(1) MAOMBI YA UMUHIMU WA KWANZA (MST. 11-24)
Katika mistari hii, tunaona maombi ya Yesu akiwaombea wanafunzi wake na wale watakaomwimini kwa sababu ya neno lao.

Kuna jambo kubwa la kujifunza hapa katika maombi ya Yesu. Katika maombi yake yote hakuwaombea wanafunzi wake wawe matajiri, au wawe na mali za dunia hii; wala hakuwaombea mambo ya mwilini yoyote. Maombi yake yote yalikuwa yanahusu mambo ya roho zao.

Aliomba kwamba Baba awalinde na yule mwovu na wawe na umoja (MST. 11, 15).
Aliomba kwamba furaha ya Yesu itimizwe ndani yao (MST. 13).
Aliomba kwamba watakaswe na kuishi maisha ya utakatifu (MST. 17),
na tena aliomba kwamba wawe pamoja naye mbinguni (MST. 24).

Yesu Kristo, hapa, anatufundisha maombi ya umuhimu wa kwanza. Hatuna budi kutamani KWANZA mafanikio ya kiroho kuliko kuwaza mafanikio ya kimwili tu. Katika maombi kwa ajili yetu na kwa ndugu zetu wengine, tuweke uzito zaidi kuomba maombi ya roho zetu zitakazoishi milele. Tuutafute KWANZA Ufalme wa Mungu na mengine yafuate baadaye.

(2) KUTOA HOJA ZENYE NGUVU KATIKA MAOMBI (MST. 11-24)
Yesu anatufundisha kueleza mambo yetu kwa ufasaha, na kutoa hoja zenye nguvu, tukieleza vizuri kwa nini tunataka tupewe sawasawa na kuomba kwetu. Tukifanya hivyo, tutaona Bwana akitujibu, maana neno la Mungu linatufundisha hivyo (ISAYA 43:26; 41:21).

(3) UWALINDE HAWA (MST. 11-12) Sisi kama wanafunzi wa Yesu, ni kondoo kati ya mbwa-mwitu (MATHAYO 10:16; MATENDO 20:29). Shetani anatafuta kuturarua na kutuondolea wokovu.

Hatuna budi kumwomba Mungu atulinde na yule mwovu wakati wote, na kuomba vivyo hivyo kwa wanafunzi wenzetu au kondoo wetu katika Kanisa. Hatupaswi kujiamini kupita kiasi na kutupilia mbali uwezekano wa Shetani kurarua wokovu wetu kwa kuwatumia mbwa mwitu wake.

Alimtumia mbwa-mwitu Delila kumrarua Samsoni aliyekuwa shujaa sana wa kiroho. Alimtumia mbwa-mwitu mkewe Uria kumrarua Daudi, mtu aliyeupendeza sana moyo wa Mungu. Aliwatumia mbwa-mwitu wengi (wanawake wageni), wakamgeuza moyo Sulemani aliyekuwa mwenye hekima kuliko yeyote mwingine mpaka akafuata miungu mingine (1 WAFALME 11:1-4).

Shetani aliwatumia mbwa-mwitu kumfanya Yuda ajinyonge baada ya kumsaliti Yesu na kumfanya Petro kumkana Yesu mara tatu. Anaweza kufanya hivyo kwetu pia tusipomwomba Mungu atulinde na yule mwovu wakati wote (MATHAYO 6:13). (

4) WAJIBU WA KUWATUNZA WATOTO WACHANGA KIROHO (MST. 12) Siku ya mwisho, kila mmoja wetu itamlazimu kutoa ripoti ya jinsi alivyowatunza watoto wake wachanga kiroho aliokabidhiwa na Mungu. Katika kumi na wawili,

Yesu aliwatunza wote isipokuwa mmoja tu aliyekuwa mwana wa upotevu. Yesu hapa anatuonyesha kielelezo cha kutimiza mapenzi ya Mungu katika MATHAYO 18:14.

(5) UMOJA ALIOTUOMBEA YESU (MST. 11, 21-23)
Watu wengine kwa kukosa maarifu, wanafikiri Yesu alituombea umoja wa madhehebu yote yanayojiita ya Kikristo.
Siyo sula la umoja au muungano wa makanisa yote linalotajwa hapa. Hatuna budi kuwa waangalifu na kuzijua fikra za Shetani.

Uomja wetu hauna budi kuwa kama umoja wa baba, Mwana na Roho Mtkatifu. Umoja wao unaambatana na Neno la Mungu katika Utakatifu wote. Baba ni Baba Mtakatifu,
(YOHANA 17:11).
Yesu ni Yesu Mtakatifu (MATENDO 4:30),
na Roho, ni Roho Mtakatifu (YOHANA 14:26).
Umoja wetu Wakristo lazima uzingatie misingi yote ya Utakatifu. Hivyo hatupaswi kuwa na umoja na watu wanaoabudu sanamu au wasioukiri wokovu.

Vivyo hivyo Umoja huu siyo kuwa kitu au kiungo kimoja, au muungano wa makanisa yote na kuwa kanisa au dhehebu moja tu, bali ni viungo MBALIMBALI vinavyotenda kazi kwa ushirikiano kama katika mwili wa mtu. Jicho linabaki Jicho, Sikio linabaki sikio n.k., lakini vyote vinashikiana bila kujali tofauti zao za kiutendaji kazi (1 WAKORINTHO 12:14, 17-20, 27). Kila Kanisa linabaki na jina na uongozi wake ila ikiwa wote tunaamini misingi ya wokovu na Utakatifu, basi tunashikiana bila kujali tofauti ndogo ndogo za kiutendaji.

(6) KUWA NA FURAHA YA YESU ILIYOTIMIZWA NDANI YETU (MST. 13)
Hatuna budi kuwa na furaha aliyokuwa nayo Yesu. Kilichomfurahisha kuliko vyote ilikuwa ni kuona watu wanaookolewa na kuishi sawa na m apenzi ya Mungu. Hii ndiyo kazi aliyoifurahia kuliko zote yaani kumpata kondoo au shilingi iliyopotea (LUKA 15:3-10).

Kuwa na furaha ya Yesu iliyotimizwa ndani yetu ni kufurahia kazi hii kuliko lolote jingine. Ikiwa tunafurahia mizaha, karata, bao, masengenyo, kazi za dunia hii n.k., kuliko kazi hii, tujue tumepungukiwa.

(7) KUCHUKIWA KWA MTU ANAYELIPOKEA NENO (MST. 14)
Awaye yote anayepewa neno la Mungu na kulipokea jinsi lilivyo na kuokolewa, sharti atachukiwa na ulimwengu, yaani watu ambao hawajaokoka.
Hatupaswi kuona ajabu tukichukiwa (YOHANA 15:24-25; 7:7).

(8) SIOMBI UWATOE KATIKA ULIMWENGU (MST. 15)
Baada ya kukutwa na magumu, Musa, Eliya na Yona; wote waliomba waondolewe katika ulimwengu kama wengine wanavyoomba. Yesu hatufundishi kufanya hivyo. Tunahitajika duniani kuangaza na kuwa chumvi ya ulimwengu na kuwahubiria walimwengu. Tukitolewa, nani ifanye kazi hii? Vivyo hivyo ni muhimu kufahamu kwamba kwa kuwa tuko duniani wazinzi na wenye dhambi wote watatuzunguka na kutushawishi tuwe kama wao.

Dawa siyo kutafuta kisiwa cha kukaa kama alivyowaza Yeremia (YEREMIA 9:2), bali ni kuushinda ulimwengu na majaribu yake ( 1 YOHANA 5:4).

(9) WAO SI WA ULIMWENGU (MST. 16)
Mwanafunzi wa Yesu hapaswi kuwa mtu anayeupenda ulimwengu na mitindo yake kama Dama (2 TIMOTHEO 4:10).

Kuwa rafiki wa dunia yaani kufanya mambo kama watu wa dunia hii, ni kuwa adui wa Mungu na kuonyesha kwamba hatujaokoka (YAKOBO 4:4; 1 YOHANA 2:15). Hatupaswi kuifuatisha namna ya dunia hii katika kujipamba, mavazi, usemi, n.k. (WARUMI 12:2).

(10) UWATAKASE (MST. 17, 19)
Wanafunzi wa Yesu walikuwa wameokoka, lakini bado walijawa na hasira, chuki (MARKO 10:41; LUKA 9:49-50, 51-55).

Aliomba watakaswe. Sisi nasi hatuna budi kuhakikisha kwamba tumetakaswa baada ya kuokolewa kwa kuomba Utakaso tukijua ni ahadi na mapenzi ya Mungu kwetu (1 WATHESALONIKE 5:23-24).

(11) KAMA ULIVYONITUMA NAMI NALIWATUMA (MST. 18)
Yesu Kristo anatuhakikishia kwamba ametutuma VIVYO HIVYO alivyotumwa na Baba. Ni neema iliyoje!
Kwa uhakikisho huu, ni muhimu kufahamu kwamba kuna uwezekano mia kwa mia wa kutenda kazi alizozitenda Yesu na kuzidi, tukiamini tu! (YOHANA 14:12).

(12) YATUPASAYO KUFANYA BAADA YA KUMJUA MUNGU (MST. 25-26)
Baada ya kumjua Mungu kwa kuzishika Amri zake (1 YOHANA 2:3-4), kila mmoja wetu anawajibika kuwajulisha wengine Jina la Yesu linalookoa tena na tena! ………………………………………………………………………………………………………………………………….. Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).

Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).

Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi.
Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu?
Jibu ni la!
Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini;
hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni.

Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6).

Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;

Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen

0767/15 445846

Ni Mimi Ndugu yako
Ev. Elimeleck S Ndashikiwe
       
elimelck@gmail.com.

0 comments:

Post a Comment