Pages

Subscribe:

Friday, 2 October 2015

THAMANI YA WOKOVU

Ufunuo 3:1 "..Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa HAI, nawe UMEKUFA".
��Kuna kisa cha kusikitisha cha binti mmoja aliyekuwa anashikiliwa na polisi akisaidia upelelezi wa tukio la mwenzie aliyemsindikiza kutoa mimba, kufia kwenye chumba cha daktari baada ya kupoteza damu nyingi. Daktari alitoloka na binti akabaki mikononi mwa polisi akidaiwa kuhusika na mauaji hayo. Jambo la kusikitisha zaidi mabinti wote walikuwa waimbaji wa kwaya ya kanisa fulani, aliyefariki aliambukizwa uja uzito na mwalimu wa kwaya, ambaye alikataa kuwa hajahusika.
��Neno la leo linasema kuna watu wanaoonekana kuwa wako hai kumbe wamekufa. Sifa moja kubwa ya mtu aliyekufa ni ufahamu kupotea, yaani milango mitano ya fahamu inakuwa haifanyi kazi. Mishipa ya fahamu ya marehemu yenye kazi ya Kusikia, Kuona, Kuonja, Kunusa na Kugusa, inakuwa imekufa. Ndivyo ilivyo kwa Mkristo au Mtu yeyote anayejiita mtu wa Mungu, huku anafurahia kufanya dhambi, mtu huyo ni Marehemu, hana fahamu, anaweza kuimba usizini tena kwa msisitizo, hata kwa kupandisha sauti juuuu, wakati yeye mwenyewe ni mkora wa mapenzi. soma - Waefeso 2:1-2.
��Mtu anaweza kuomba "Utusamehe dhambi zetu kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea", baada ya Ibada utasikia akisema "mtu fulani amenitoka sitaki hata kumuona", kuna watu hawapendi kutokana na kasoro zao au basi wivu tu.
Marehemu kiroho, anaweza kuimba wimbo wa kukemea dhambi, akimaliza utashangaa, hasira juu, ugomvi, masengenyo, uongo, wivu, husuda, mahaba na kila uchafu unaotendwa kwa siri.

Ukiwaona watu wanajaa kwenye majumba ya Ibada, wakiimba mapambio ya kuabudu na kusifu, unaweza kudhani ni wacha Mungu, kumbe ni marehemu, hawakomi kutenda dhambi.
��Laana, vilio, majuto, kukosa amani na matumaini, mikosi na dhoruba mbalimbali zinazoikumba jamii yetu ni kutokana na Marehemu wanaotembea kuzidi kuongezeka katika majumba ya Ibada.
Dhambi zinakata 'Network' kati yetu na Mungu, marehemu akiomba Mungu anacheka wala hasikii (Mithali 1:22-31), japo shetani anaweza kujibu maombi wakifikiri ni Mungu, na wakaendelea hadi kufia dhambini na kupotea milele. ��Haya vijana kwa wazee! Wakati umewadia tena wa kuunganishwa na Mungu, yatosha kuishi maisha yaliyo chini ya viwango vya mbinguni, na kuendelea kuwa chini ya mamlaka ya adui kwa hila. Mlango wa rehema ungali wazi, ni fulsa ya kila mmoja kuokolewa na kupewa ushindi daima.
BWANA AWAANGAZIE NURU YA USO WAKE NA KUWAPA AMANI. NAWATAKIA SIKU NJEMA.

Ni mimi rafiki yenu mpendwa
Ev. Elimeleck S Ndashikiwe
elimelck@gmail.com

WANAWAKE WA INJILI (W.W.I) WANATAKIWA KUIDHIHIRISHA IMANI YAO

Hivyo ni lazima Mke kama Mke uwe ni mwanamke wa IMANI DHABITI.

2 Timotheo 1:5-6
Kijana anayetajwa katika  mlango huu, aliishika imani aliyokuwa nayo  mama yake, lakini mama wa kijana huyu naye aliishika imani  iliyokuwa kwa mama yake pia.

Hivyo bibi ameweza kumfundisha mwanawe  imani, na mwana naye akamfundisha  mwanawe imani. Hivyo tunaona umuhimu wa mke kuwa na imani inavyoweza kuambukiza watoto na hata wajukuu.

Na kama mke ukiwa  mjuzi wa Mambo ya Mungu na kuweza kuambukiza watoto IMANI ILIYO DHABITI, hakuta kuwa na sababu ya watoto kutanga tanga wawapo wakubwa. Watoto watatanga tanga wakijua Imani ya wazazi haikuwa na matunda yoyote, hivyo ni rahisi kuiupuuza imani hiyo. Lakini watoto wakiona Imani ya wazazi inaheshimiwa, inazaa matunda sio rahisi watoto kuiacha imani hiyo.

NI LAZIMA SASA MAMA KAMA MLEVI WA FAMILIA NA MJENZI WA NDOA IMANI YAKO IWE DHABITI NA IMARA. Ni lazima uwe mtu wa kupenda:
1 . Kuhurudhia Ibada.
2. Kusoma neno la Mungu.
3. Kushika taratibu za Dini yako katika Imani yako.
4. Kuwafundisha watoto   Imani  hiyo  kwa kumaanisha.
5. Kupenda kufunga na Kuomba kila mara.

Lakini pia kutoa sadaka  kwa Mungu.

FAIDA ZA KUWA MKE WA IMANI.
Faida ziko nyingi sana, hata kila mmoja ni shahidi, na kila anayejua Faida za kuwa na imani thabiti akiamua kuorodhesha nafasi haitatosha. Pamoja na kuwa na faida nyingi sana hizi hapa ni moja ya faida hizo.

1. Kuwa mwanamke wa Hekima na Adabu. Utajikuta umekuwa mwanamke wa hekima na adabu tele, hii ni kwa sababu umekuwa karibu na Imani yako ambaayo ina Mungu ndani yake. Tena utakuwa mwanamke wa Maarifa,, Kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa. Na ukishakuwa mtu wa maarifa hakuna kitakachokushinda kwani Kwa hekima ambayo Mungu atakujalia basi utajikuta unaweza kukabiliana na changamoto nyingi katika maisha lakini pia katika ndoa. Hutakuwa mtu wa kukosea kosea na kufanya uzembe ama kukurupuka , utakuwa mtu wa Utaratibu na mtu wa staha na kuweza kujiendesha.

2. Mumeo atakuheshimu . Katika maisha ya ndoa mara nyingi wanawake wamekuwa wakilalamika kutoheshimiwa, kutothaminiwa na kupuuzwa ama kuumizwa,

Faida moja wapo ya kuwa mwanamke wa Imani Thabiti ni pamoja na Mume kukuheshimu,, kukuthanini na kukupenda.

Hii haitakua na mjadala, kwani moja kwa moja kwa Imani yako itakufundisha nini wajibu wako kama mke, nini unapaswa kufanya. Wakati mwinigne Mume anakushinda na amekuwa kwazo kwako sana,,   

umemshtaki kwa wadhamini, kwa wazazi, kwa  marafiki zake , kwa boss wake, kwa kaka zake,  Ustawi wa jamii, mahakamani, kote huko lakini bado tu hasikii na wewe unampenda na kuipenda ndoa yako… Sasa  ni lazima uwe na Imani Thabiti ili iweze kukusaidia. Imani Thabiti haishindwi  na jambo lolote lile. Lakini kwa kuishika Imani yako vyema na Kumheshimu Mungu ipasavyo. Ni lazima Mumeo atakuwa na hofu ndani yake . Na atakupenda na kukuheshimu, Sio kwa vile unamlazimisha afanye hivyo la hasha, Lakini kutakuwa na Nguvu ya namna yake itakayomsukuma kukupenda, kukuheshimu na kukuthamini,
Ni kama ATAMUONA MUNGU katika maisha yako, Na atakuwa na hofu ya kukutenda mabaya. 3. Kufanikiwa katika kila idara. Kwa vile utakuwa mwanamke wa Imani, basi Mungu atakuwa pamoja na wewe. Utafanikiwa sana katika idara zote, kiuchumi,, kiimani kiroho na kimwili. Hutakuwa mtu wa kuwa mkia, bali utakuwa mwanamke wa kuwa Kichwa na mafanikio yataambatana na wewe katika kila Nyanja. Mumeo atakuita Heri, lakini watoto wako pia watakuita Heri, kwani utakuwa mwanamke mwenye Hekima na Adabu.                                                 

Mithali 31: 30 “Upendeleo hudanganya, na Uzuri ni Ubatili, Bali mwanamke Amchaye Mungu ndiye atakayesifiwa”   MWANAMKE ANAPASWA KUFANYA MAMBO GANI KATIKA KUMTUKUTA MUNGU. Badala ya kupoteza muda katika kukaa bar, kunywa pombe, kuzurura na kusogoa ni bora sasa mwanamke uwe mwanamke wa Busara na Utii wenye Adabu. Yako mambo mengi ambayo mwanamke kama mwanamke anapaswa kufanya. Lakini katika hayo mambo mengi, mambo makuu ni haya:
1. Kuomba. 2. Kufunga. 3. Kukarimu. Mwanamke amejaliwa Roho ya Huruma, na uvumilivu na staha, na ndio maana Mungu akaona ni vyema mwanamke aweze kuitwa mama, Abebe ujauzito, Azae, na kunyonyesha, MWANAMKE HAPA ALIONEKANA ANA HURUMA NA UVUMILIVU.
Hivyo basi ni lazima mwanamke uwe muombaji, Tena muombaji wa kuombea mambo mengi. Kujiombea Mwenyewe, kuiiombea Familia lakini na Taifa lako kwa ujumla. Lakini pia Maombi ya Kufunga ni Yamuhimu na yana nguvu. Kila mwanamke anapaswa kwua muombaji wa kufunga pia. Mwisho kabisa mwanamke anapaswa kuwa mtu wa kukirimu, sio mchoyo, sio mtu wa upendeleo wala ubaguzi. Lakini ni lazima mwanamke awe mkarimu. Kwa familia yake lakini na kwa watu wanaomzunguka. Mifano tunayo mingi ya wanawake wacha Mungu walivyofanya. Walikarimu, waliwavika watu nguo waliwapa watu chakula na kuuguza wenye majeraha. Kwa kufanya hivi kwa Kukarimu Unaweza Kumkarimu Mungu bila kujua. Hivyo ni wajibu wa Mwanamke kutokuwa Mchoyo. MWANAMKE UKIFANYA MAMBO HAYA LAZIMA UTAFANIKIWA SANA NA ROHO WA MUNGU ATAKUWA KARIBU NA WEWE.

Ni mimi rafiki yako
Ev. ELIMELECK S NDASHIKIWE
  Tel:- 0767445846
           0715445846
elimelck@gmail.com

Thursday, 1 October 2015

NGAO YA IMANI

KUISHI MAISHA YA IMANI KTK ULIMWENGU USIOAMINI

Kuishi maisha ya imani maana yake ni kuwa kwa kipindi chote cha maisha yetu hapa duniani, kwa kipindi chote cha uhai wetu, na kwa namna yoyote ile inayoashiria maisha kama kuongea kwetu, kutenda kwetu, kuwaza kwetu, kuenenda kwetu, kuvaa kwetu, kula kwetu, kuona kwetu, kukiri kwetu, kutoa na kupokea kwetu, kufanya kazi kwetu, lupigana kwetu, kushinda kwetu, kuomba kwetu na hata namna yote ile ya kuwajibika kwetu kwa watu wengine tunayafanya haya yote kwa imani. Tunayafanya haya yote kwa uhakika kabisa, kwa kutokuwa na mashaka wala hofu, tunayafanya kama vile tumejua mwisho wake hata kama hatujayaona kwa macho yetu bado.

Kama kuna mambo tunatarajia katika kuishi kwetu, basi kuishi kwa imani katika hayo tunayoyatarajia ni kuishi tukiwa na uhakika na udhihirisho ya kuwa hayo mambo yatatokea na kufanyika halisi maishani mwetu bila kujali changamoto zitokanazo na imani yetu katika mambo hayo.

Katika tafsiri ya kitabu cha Waebrania 11:1, “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”.

Kwa lugha nyingine naweza kusema, imani ni udhihirisho wa mambo ninayoyatarajia kuyapata, mambo ninayotumaini kuyapata, mambo ninayotamani na kuwa na shauku nayo katika maisha yangu.

Kwa hiyo naishi kwa namna inayodhihirisha na kuthibitisha kabisa kuwa kuna mambo ninayoyangojea hapo mbele. Kama imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, hii inamaanisha kuwa ni muhimu sana kuyajua hayo mambo yatarajiwayo ni mambo gani kwasababu siwezi kuwa na imani na kitu nisichokijua. Kwa mfano, siwezi kuwa na imani kama Yesu Kristo atarudi tena wakati simjui Yesu mwenyewe wala jambo lolote kuhusu yeye, siwezi kusema nina imani Yesu ataniponya wakati hata sijawahi kusikia habari za Yesu na kwamba yeye ana uwezo wa kuponya

Hivyo ni lazima niwe nimesikia habari za jambo Fulani, ni lazima niwe nimeyajua hayo mambo ninayoyatarajia ili niseme sasa nina imani nayo kwamba yatatokea kwangu.

Ninachosema hapa ni hiki, kwa sababu imani chanzo chake ni kusikia, ni muhimu sana kujua unasikia juu ya nini.

Kila mtu hujenga imani ya kile anachokisikia na zaidi sana kile achokifahamu na kukijua. Ukisikia sana habari za waganga basi utajenga imani yako kwa waganga lakini kitu cha kujua hapa ni kuwa kama wewe ni raia wa ufalme wa Mungu basi ni lazima imani yako iwe katika mambo yatokanayo na ufalme huo.  Neno la Kristo ndio msingi wa kujenga imani ya kweli kwa kila aaminiye kwa moyo wake na kukiri kwa kinywa chake kwamba Yesu ni Bwana. Kwa hiyo kama nimeamua kuishi maisha ya imani ndani ya Yesu, ni lazima nizidi kumsikia sana Yesu ili nizidi sana kujenga imani yangu kwake kwenye mambo ninayotarajia.  Kabla sijajua kuwa Yesu ni mwokozi nilimdharau na kuwakejeli wote walionambia habari zake, kwa hiyo nisingeweza kuishi maisha ya imani wakati huo. Nilipomjua Yesu ni nani, kwa kusikia, nikajenga imani yangu na kuanza kutarajia mambo kadha wa kadha yaliyondani yake yeye. Kwa hiyo hakika ya mambo yatarajiwayo inakuja kwa kuzidi sana kuongeza ufahamu katika kuyajua hayo mambo yaliyofungwa ndani yake yeye ninayemwamini. 

Mambo yatarajiwayo, kwa tafsiri niliyoiweka hapo juu, inamaanisha mambo ninayotumainia ndani ya imani yangu katika Kristo na haya mambo ni kama:  Uzima  Uponyaji  Baraka za mwilini na za rohoni  Mafanikio na maendeleo  Maisha ya ushindi  Ulinzi  Uzima wa milele  Masomo  Chakula  Mavazi  Nguvu  Kwa kuchukua mfano mmoja hapo juu, mimi nimeokoka ingawa nimekuwa naishi maisha ya hali ya chini kiasi kwamba hata mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi na hata mahali pa kulala sina, kuishi maisha ya imani katika hali hii ni kuwa na hakika juu ya hayo mambo ninayoyahitaji kuwa nitayapata kutegemeana na imani yangu katika yeye ninayeamini, yaani Kristo, kuwa anaweza kunipa hayo yote sawa sawa nay ale ninayoyafahamu na kuyajua, yale niliyoyasikia amesema kuwa atanifanyia. 

Ingawa mwili wangu utaonekana kuchakaa lakini imani yangu inanipa nguvu na tumanini kwani ninajua kabisa kuwa ipo siku Yule ninayemwamini atayabadilisha maisha yangu kwa kadri ya imani yangu, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yangu na zaidi sana kwa kadri ya utajiri wa utukufu wake.  Kwa upande mwingine, kuna mambo yasioonekana ambayo nayo tunatakiwa tuishi kana kwamba tumeyaona na hapa Neno la Mungu linasema, Imani ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Neno bayana ni sawa na kusema halisia, imani ni uhalisia, waziwazi au inayooneka kabisa kwa macho ya nyama na damu.

Umesubiria mtoto kwa muda mrefu, imani inakupa nguvu na tumaini la kuendelea kuishi maisha yako kila siku kama mama aliyepata mtoto tayari.  Bayana. Halisia. Inayoonekana. Kama kuna jambo lolote lile ninalolingojea na bado sijaliona, ninatakiwa niwe nalingojea kama vile nimeshaliona kama vile Babu Ibrahimu, habari zake zinasema alitarajia yasiyoweza kutarajia, alitarajia mambo yasiyoonekana kana kwamba yameonekana, alimtarajia Isaka wakati hali yake na ya Bibi Sara haikuwa na uwezo wa kuwapa motto.Lakini yeye alisubiri katika kutarajia kwake mambo yasiyoweza kutarajiwa kabisa.

Nguvu ya imani yake aliipata kwa kumjua anayemwamini.   “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani na ndivyo mema yatakavokujia”, ndivyo utakavyozidi kupata ushindi maishani mwako, ndivyo utakavyozidi kushinda vita na makwazo ya duniani hapa na ndivyo utakavyozidi kuishi maisha yenye utulivu na usalama kwa maana unamjua yeye akupaye nguvu za hata kupata utajiri.  Kwa hiyo kuishi maisha ya imani ni katika hali zote kwa maana pasipo hiyo imani haiwezekani kabisa kumpendeza Mungu kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima, sio ombi, lazima aamini (awe na hakika wa mambo anayotarajia toka kwake) kwamba yeye Mungu yuko na zaidi ya hayo huwapa thawabu, huwapa Baraka, huwapa mambo mema, huwapa mafanikio, huwapa hazina njema wale wote wanaomtafuta. Katika hali zote, kufanikiwa au kutokufanikiwa, kupata au kukosa, raha au mateso. 

Imani inahitajika na hivyo wakati wa Furaha wewe furahi kwa imani na wakati wa majaribu ya imani yako usiseme hii sio imani kwani ni vema kuhesabu ya kuwa ni Furaha tupu tunapoingia katika majaribu mbali mbali tukijua kuwa kujaribiwa kwa imani yetu huleta saburi maishani mwetu. Kwa hiyo neno imani lina maneno matano ambayo ni: 

1. Hakika-kutokuwa na shaka wala hafu, thabiti 
2. Mambo-ahadi za Mungu unazozijua kama Neno lake linavyosema 
3. Yatarajiwayo-tumaini la kungojea na kusubiri 
4. Bayana-halisia, inayoonekana
  5. Yasiyoonekana-kwa macho ya nyama na damu 

Kwa hiyo, ninapomalizia ukurasa huu, napenda kusema kuwa kuishi maisha ya imani ni kuishi maisha tegemezi katika kile anachokisema Mungu.
Ni kuishi maisha ya mtu wa haki, mwenye haki anaishi kwa imani, anaishi kwa kuwa na ujasiri na uhakika wa mambo yote anayoyatarajia hata kama hajayaona kwa macho yake. Tunawaza kwa imani, tunaongea kwa imani, tunakula kwa imani, tunatembea kwa imani, tunafanya kazi kwa imani, tunaomba kwa imani, tunaangalia kwa imani, tunaenenda kwa imani na kwa ujumla wake yote tunayoyafanya iwe ni kwa neno au kwa tendo tunayafanya yote kwa imani katika jina la Yesu tukizidi sana kumshukuru Mungu Baba.  Kwa maana tunajua ya kuwa pasipo imani, haiwezekani kumpendeza Mungu kwani sisi kama wenye haki imetupasa kuishi kwa imani. Kuna uhusiano kati ya kuwa mwenye haki na kuishi maisha ya imani. Haiwezekani mtu akaishi kwa imani bila kuhesabiwa haki katika Yesu Kristo aliye mwanzilishi wa imani yetu.

Na huu uhusiano ndio tutakao uchambua na kujifunza juu ya kwa nini mwenye haki aishi kwa imani. Umebarikiwa katika jina la Yesu Kristo! –

Ni mimi rafiki yako Ev. ELIMELECK S NDASHIKIWE

0767445846  &
0715445846.
elimelck@gmail.com