Thursday, 8 October 2015
AGANO LA SABATO
KUANGUSHA NGOME YA MAWAZO
Mitume na manabii waliotangulia zamani tunaona kabisa kuwa walifanikiwa mbele za MUNGU baada tu
ya
kufanikiwa kuzijua mbinu za shetani
ambazo mara nyingi huzitumia kuachilia mawazo ndani ya mtu.
Aidha,
mgawanyiko wa mawazo haya una chimbuko lake maalum.
Mawazo chanya ambayo ni mema chimbuko lake ni Mungu ambaye amejitambulisha katika maandiko matakatifu ya Biblia; na mawazo hasi ambayo ni mabaya na maovu chimbuko lake ni Shetani na Ibilisi. Ninaposema chimbuko la “mawazo chanya” ambayo ni mema asili yake ni Mungu, hii ni kwa mujibu wa Biblia jinsi alivyomtafsiri Mungu kwamba anayo mawazo anayotuwazia binadamu wake kama livyoandikwa:
“Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” (Yer.29:11)
Aidha ninaposema “mawazo hasi” ambayo ni mabaya na maovu asili yake ni Ibilisi na Shetani, hiyo nayo ni kwa mujibu wa Biblia kama Yesu alivyomtambulisha Shetani kwetu akisema:
“Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yee ni mwongo na baba wa huo.” (Yh.8:44) Unaona maneno kama haya ya “yeye ni mwuaji tangu mwanzo…” na “…asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa sababu yeye ni mwongo na baba wa huo…” haya yote ni mambo mabaya, ambayo chimbuko lake ni “mawazo hasi” yaliyomo katika “mfumo wa mawazo” katika akili za Ibilisi.
Sasa basi, ili kukujengea mtiririko mzuri wa uelewa katika hoja hii makini, sina budi kukujulisha pia kwamba, hata mambo ya kiroho yanayohusu imani kwa Mungu, au kutokuamini Mungu nayo pia yako katika mfumo wa mawazo!
Biblia inaposema imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yalisiyoonekana, maana yake “hayo mambo yatarajiwayo” yako katika “mfumo wa mawazo”.
Mawazo huonekana akilini na rohoni tu. Na hakika juu ya mawazo yaliyoko moyoni nayo inategemea na akiba ya “mawazo ya Neno la Mungu” iliyoko ndani ya moyo wa mtu. Haya, hali ya “kutokuamini” nayo iko katika mfumo wa mawazo moyoni mwa mtu. Ndiyo! Kutokuamini ni akiba ya “mawazo hasi na yaliyo kinyume neno la Mungu”!
“Kutokuamini” ni “mtazamo kinyume na kufanikiwa kwa kutegemea njia za Mungu na kanuni zake”. Kwa hiyo, “Imani kwa Mungu” na “kutokuamini” vyote viko katika mfumo wa mawazo lakini, moja liko kwenye fungu la mawazo chanya kwamba ahadi za Mungu ni kweli na ndivyo ilivyo; na “kutokuamini” ni fungu la mawazo hasi yaliyojaa mashaka na wasiwasi juu ya uaminifu wa Mungu na ahadi zake.
Kupitia makala haya, tutakwenda kuchunguza ukweli kuhusu nguvu za mawazo, faida na athari zake katika maisha ya binadamu hapa duniani. Ngome za mawazo Sasa baada ya kupata utangulizi kuhusu tafsiri pana ya mawazo, mgawanyiko wake na chimbuko la mgawanyiko huo, ni bora sasa tuingie sehemu nzito kuhuzu mawazo ambayo yameitwa ngome katika maandiko matakatifu kama ilivyoanidkwa: (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)
tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; (2 KOR.10:4-5)
Hapa tumesoma maneno ya “silaha za vita”, “kuangusha ngome” na “kuangusha mawazo”. Kabla sijaingia uchambuzi wa ngome za mawazo hebu nitoe tafsiri ya msamiati wa neno “ngome”. Ngome ni ukuta mnene uliojengwa kwa madhumuni ya kuzuia kuingia ndani, hasa maadui kuingia ndani kwa urahisi.
Kabla ya kuingia ndani ya mji/nyumba ili kupigana na kuteka waliomo/vilivyomo ndani kazi ya kwanza ni "kuangusha ngome za kuta” Haya, tuje kwenye tafsiri ya msamiati wa “ngome za mawazo” kwa mujibu wa maandiko tuliyosoma hapa juu. Kwa kifupi, maandiko yalichokuwa yana kilenga hapa ni
1. “Falisafa za kibinadamu” zilizotungwa kwa kusudi la kupingana na elimu ya Neno la Mungu m.f nadharia ya mabadiliko inapopingana na “sayansi ya uuumbaji”
2. “Nadharia potofu ya kidini” yaliyotungwa kupingana na kweli ya Neno la Kristo m.f hakuna kuokoka wala kuwa mtakatifu duniani, Roho na karama zake vilikwishakoma Kwa mujibu wa maandiko tuliyosoma, tunagundua mara moja kwamba Ibilisi ndiye mwasisi na mjenzi wa “ngome za mawazo” na mikakati yake siku zote ni kutanguliza mapema “Mawazo yake hasi” katika fahamu za watu ili kuwejengea “Falsafa za kibinadamu” zilizo kinyume na elimu ya Mungu pamoja na “mafundisho potofu ya kidini”
Hapa, kusudi la Ibilisi la kuwajengea mapema watu “ngome za mawazo” ni ili ziwazuie waathirika kuipokea Injili ya Kweli na Neno la Mungu (Biblia) na kupata kuokolewa na kujazwa Roho Mtakatifu. Na ndiyo maana sababu kubwa ya watu wengi kutokuiamini Injili sahihi ya wokovu ni kwa kuwa Shetani alitanguliza kwenye akili zao hizi i) Falisafa za uongo uliohalalishwa kijamii na ii) Injili za uongo zilizohalalishwa kidini!
Tutafanikiwa tu endapo tutazijua mbinu za Ibilisi
mara nyingi
huitumia NGOME YA MAWAZO
kama
silaha kuu.
MUNGU WANGU WA MBINGUNI AKUBARIKI KWA KUUSOMA UJUMBE HUU
naamini utakuwa umebarikiwa sana.
Ni mimi ndugu yako ktk Kristo
Ev. Elimeleck S Ndashikiwe
elimelck@gmail.com
0767445846 &
0715445846
NGAO YA IMANI
UMUHIMU WA KUWEKA IMANI YAKO KATIKA JINA LA YESU KRISTO “Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali , saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. KWA JINA LA YESU KRISTO WA NAZARETI, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.
Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda …” (Matendo ya Mitume 3:1 – 8) Ukifuatilia historia ya kilema huyu aliyeponywa utaona ya kuwa alikuwa hivyo tangu kuzaliwa, na alipopona alikuwa na umri uliopita miaka arobaini (M Na ndivyo ilivyokuwa wakati kilema huyu alipopona, watu waliokuwa hekaluni waliwashangaa wakina Petro na Yohana kama vile kilema huyo alipona kwa uwezo wao. Petro alipoona hali hiyo, aliamua kuwaeleza watu hao ukweli ulivyo; alisema hivi; “Basi (Yule aliyekuwa kilema) alipokuwa akiwashika Petro na Yohana, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile lililoitwa tao la Sulemani, wakishangaa sana. Hata Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kama kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi au kwa utauwa (utakatifu) wetu sisi?” (Matendo ya Mitume 3:11 – 12). Petro alikuwa anafanya jambo muhimu hapa kwa kusaidia kubadilisha mawazo ya watu ya kufikiria kuwa uwezo uliomponya kilema ulikuwa ni wa Petro na Yohana ambayo haikuwa si kweli. Kama uwezo huu haukuwa wao, muujiza huu siri yake ni nini? Petro aliendelea kusema hivi; “Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa Baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu ….. Na kwa IMANI KATIKA JINA LAKE, JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele zenu ninyi nyote” (Matendo ya Mitume 3:13 – 16). Hebu tafakari maneno haya ya Petro; “Na kwa IMANI KATIKA JINA LAKE JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU….” Wakina Petro na Yohana waliweka imani yao katika jina la Yesu Kristo. Walikuwa na uhakika mioyoni mwao kuwa siri ya miujiza imo katika jina la Yesu Kristo – ndiyo maana walipomkuta huyo kilema walimwamuru asimame kwa jina hilo! Weka imani yako katika jina la Yesu Kristo ukitaka kuona ishara na miujiza ya Yesu Kristo maishani mwako na kwa wale unaowahudumia pia. Wakijua hili wanafunzi wa kwanza wa Yesu Kristo walipokatazwa “wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu” na Anasi kuhani mkuu, waliomba wakasema; “…Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ISHARA NA MAAJABU vifanyike kwa JINA LA MTUMISHI WAKO MTAKATIFU YESU” (Matendo ya Mitume 4:18,29 – 31) Ni muhimu kuwaeleza na kuwakumbusha watu umuhimu wa kuweka imani zao katika jina la Yesu Kristo wakitaka kuona mkono wa Bwana ukiponya, ukifanya ishara na miujiza. Nakumbuka kuna mama mmoja alifika nyumbani kwangu akiwa anaumwa sana toka mkoa mwingine nje ya mkoa huu wa Arusha ninaokaa. Baada ya mahojiano naye nilifahamu ya kuwa ameugua bila kupona kwa muda wa miaka miwili. Na katika miaka hiyo miwili amezunguka kwa watu mbalimbali kuombewa bila mafanikio. Alipoona haponi akaenda kwa waganga wa kienyeji ambako nako hakupona. Alipoona kwa waganga wa kienyeji haponi akaanza kutafuta watu wamuombee tena. Katika mazungumzo hayo nilitambua kuwa anapokwenda kuombewa anaweka imani yake katika watu wanaomuombea na wala haweki imani yake katika jina la Yesu Kristo. Nilifungua Biblia yangu na nikaanza kuzungumza naye juu ya uweza wa jina la Yesu Kristo, na umuhimu wa yeye kuweka imani yake katika jina la Yesu Kristo na siyo kwangu. Mwishoni nikamuuliza kama ameelewa na ikiwa yuko tayari kwa maombi kwa kulitumia jina la Yesu Kristo. Yule mama akajibu akasema; “Ndiyo nipo tayari kwa kuombewa, naamini kwa jina la Yesu Kristo nitapokea uponyaji” Mara nilipoanza kuomba, aliangushwa chini na mapepo yaliyojidhihirisha toka ndani mwake. Nikayaamuru mapepo hayo yamtoke mama yule kwa JINA LA YESU KRISTO – na mara hiyo yakamtoka na akawa mzima! Ugonjwa uliomsumbua kwa muda wa miaka miwili ulitoweka, yule mama pamoja na mume wake aliyemsindikiza waliondoka kwa furaha huku wakimsifu Mungu kwa matendo makuu aliyowatendea. Kumbuka Petro alisema; “… Kwa IMANI katika JINA LAKE (YESU) , JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU ….” Atakayeliitia jina la Bwana ataponywa : Nabii Yoeli alitabiri kuwa; “Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote ATAKAYELIITIA JINA LA BWANA ATAPONYWA; kwa kuwa …. Watakuwako watu watakaookoka, kama Bwana alivyosema;” (Yoeli 2:32). Mtume Paulo alitilia mkazo utabiri huu aliposema; “Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, KILA ATAKAYELIITIA JINA LA BWANA ATAOKOKA (Warumi 10:12 – 13). Kila anayeliitia jina la Bwana Yesu kwa imani anaponywa na, anaokoka kwa kuwa ndani ya jina hili la Yesu Kristo mna uponyaji na wokovu kwa kila amwaminiye Yesu Kristo. Lakini Mtume Paulo anauliza swali muhimu ambalo ni vizuri kulitafakari; anasema; “Basi wamwitaje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? (Warumi 10:14). Hili jambo ni kweli. Huwezi kumwita mtu usiyemwamini. Hii ina maana ya kuwa ikiwa tunataka watu waliitie jina la Yesu ili waokoke na kuponywa madhaifu yao, inatubidi tuhubiri na kufundisha juu ya Yesu na jina lake. Ndiyo maana Bwana Yesu Kristo alimwambia Anania ya kuwa Paulo “ni chombo kiteule kwangu, ALICHUKUE JINA LANGU, mbele ya Mataifa, na Wafalme, na wana wa Israeli” (Matendo ya Mitume 9:15). Biblia inasema pia kuwa; “Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, AKAWAHUBIRI KRISTO. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosewa na Filipo, walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule” (Matendo ya Mitume 8:5 – 8). Smithi Wigglesworth aliyekuwa mhubiri wa huko Uingereza katika miaka ya 1930 aliwahi kushuhudia katika mahubiri yake kuwa siku moja aliitwa kwenda kumuombea mgonjwa mmoja wa kifafa aliyekuwa amezidiwa hata kushindwa kuamka. Anasema watu wa eneo lile na hata ndugu zake yule mgonjwa walikuwa wamekata tamaa. Waliona ndugu yao atakufa kwa ugonjwa huo. Kwa hiyo ilimchukua muda Bwana Smith Wigglesworth kupata walio tayari kushirikiana naye katika kumuombea mgonjwa yule. Mwishoni alifanikiwa kuwapata, na anasema walikizunguka kitanda cha yule mgonjwa na wakaanza kuliitia jina la Yesu kwa pamoja wakisema “Yesu, Yesu, Yesu, Yesu,….” Kwa kulirudiaruda jina hili. Baada ya kuliitia jina la Yesu kwa muda hivi, anasema nguvu za Mungu zilishuka kitandani kwa yule mgonjwa, zikamtingisha mgonjwa na kitanda chake. Yule mgonjwa akapona saa ile ile, akavaa nguo na kutoka nje. Kijiji kizima kilitaharuki na kushangaa kilipomuona mtu yule amepona. Smith Wigglesworth alipoona watu wamekusanyika hivyo wakishangaa, alichukua Biblia yake akahubiri, na watu wengi walikata shauri na kuokoka siku ile. Ni muhimu ufahamu ya kuwa muujiza unaofanywa kwa jina la Yesu Kristo unawavuta watu kwa Yesu Kristo, wamwamini na kumfuata. Ndiyo maana imeandikwa juu ya Yesu Kristo kuwa; “Hata (Yesu Kristo) alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi WALIIAMINI JINA LAKE, walipoziona ishara zake alizozifanya” (Yohana 2; 23). Siku moja nilikuwa katika sehemu fulani nikifundisha juu ya jina la Yesu Kristo. Mwisho wa somo nilisema watu wanaotaka kujazwa na Roho Mtakatifu na wanene kwa lugha mpya pamoja na wagonjwa waje mbele. Watu wengi walikuja mbele. Niliwaambia hatutaomba neno lolote zaidi ya kuliitia jina la Yesu kwa pamoja na kwa kulirudiarudia. Kwa pamoja tukaanza kuliitia jina la Yesu tukisema kwa sauti; “Yesu, Yesu, Yesu, Yesu…..” Muda haukupita mwingi, tukiwa bado tunaliitia jina hili nikasikia toka upande wangu wa kushoto sauti ya maji mengi yakiporomoka. Nilijua hii ni ishara ya uwepo wa Roho Mtakatifu kwani mahali tulipokuwapo hapakuwa na mto wowote karibu, wala mvua ilikuwa hainyeshi. Baadaye nilipowaeleza watu juu ya sauti hiyo ya maji, kuna wengine pia waliosema kuwa waliisikia. Tulipoendelea kuliitia jina la Yesu Kristo, wagonjwa walipona, waliokuwa na mapepo walipona, na wengine walijazwa Roho Mtakatifu na wakazungumza kwa lugha mpya. Ishara na miujiza mingi ilifanyika kwa kuliitia jina la Yesu Kristo. Kumbuka Yesu Kristo alisemal “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo, watasema kwa lugha mpya…” (Marko 16:17 –18). Hukumu kwa kutoliamini jina la Yesu : “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu HAKULIAMINI jina la Mwana pekee wa Mungu” (Yohana 3:18). Usipoliamini jina la Mwana pekee wa Mungu – jina la Yesu Kristo ujue umekwisha kuhukumiwa. Hii ina maana ya kuwa unapoteza wokovu; - unapoteza ushindi; - unapoteza uzima wa milele; - na pia bado unakaa katika mauti! Hebu soma na kutafakari mistari ifuatayo ili uone umuhimu wa kuliamini jina la Yesu Kristo: “Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lolote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba TULIAMINI JINA LA MWANA WAKE YESU KRISTO, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri” (1Yohana 3:21 – 23). “Bali wote waliompokea (Yesu Kristo) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale WALIAMINIO JINA LAKE” (Yohana 1:12). “Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu; hiyo imani yetu. Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? …. Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa, mna uzima wa milele, ninyi MNAOLIAMINI JINA LA MWANA WA MUNGU” (1Yohana 5:4-5; 11 – 13). “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana JINA jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” (Matendo ya Mitume 4:12) – isipokuwa ni JINA LA YESU KRISTO! MUHIMU : Kama tulivyokwisha kukuandikia katika sura ya tatu ya somo hili – ukitaka kulitumia jina la Yesu Kristo kihalali na uweze kuona uwezo na mamlaka yake ni muhimu: Kwanza: Uwe mwana wa Mungu kwa kumpokea Yesu Kristo moyoni mwako kama Bwana na Mwokozi wako; Pili: Uwe mtii ukifuata maagizo ya neno la Kristo katika Roho Mtakatikfu. Kuna watu wengine wanataka kuwa watii kufuata maagizo ya neno la Kristo huku hawapendi kuokoka. Hawajui utii bila kuokoka ni utii nusu – ukitaka uone muujiza wa jina la Yesu Kristo katika maisha yako inabidi ufanye yote mawili – uokoke na utii. Ikiwa hujaokoka na unataka uokoke sasa isome sala ifuatayo kwa sauti (ikiwezekena upige magoti) mahali pa utulivu huku ukiamini ya kuwa Mungu anakusikia: “Ee Mungu wangu Mtakatifu. Nimesikia neno lako nami nimeamini. Naomba unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha yangu yote. Damu ya Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yangu, naomba initakase sasa katika roho yangu, nafsi yangu na mwili wangu. Nimefungua moyo wangu sasa; Ee Bwana Yesu Kristo nakuomba uingie ndani yangu, uwe Bwana na Mwokozi wangu kuanzia sasa na siku zote. Ahsante kwa kunisamehe dhambi zangu na Ahsante kwa kuniokoa. Amina” Ikiwa umeisema sala hii kwa imani, basi sasa wewe umeokoka na dhambi zako zimesamehewa na kusahauliwa na Mungu sawasawa na alivyoandika katika neno lake. Jina la Yesu Kristo ni halali yako kulitumia!