Pages

Subscribe:

Thursday, 8 October 2015

AGANO LA SABATO

WAKRISTO WENYE IMANI YA SABATO Neno SABATO linatokana na neno la lugha ya Kiebrania liitwalo SHABBATH, au SABBATON kwa lugha ya Kiyunani, likiwa na maana ya "KUKOMA, au KUTULIA, au KUSTAREHE au PUMZIKO." Kwa asili SABATO ilianzia pale Mungu alipomaliza kazi ya uumbaji. Biblia Takatifu inasema kwamba: "Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya." - (Mwanzo 2:2-3) Kama tulivyotangulia kujifunza maana ya SABATO ni "KUKOMA, au KUTULIA, au KUSTAREHE, au PUMZIKO" ndiyo maana tumeona "...Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba..." - (Mwanzo 2:2-3). Mungu mwenyewe alipumzika "...alistarehe..." baada ya kumaliza kazi Yake ya uumbaji. Kutokana na umuhimu wa kupumzika Kwake; Mungu akaitakasa siku hiyo ya saba. Neno "TAKASA" maana yake ni "KUWEKA WAKFU au KUTENGA KWA AJILI YA MATUMIZI MATAKATIFU. Baada ya uumbaji, kuanzia wakati wa Adamu hadi Yusufu mwana wa Yakobo (Israeli), kwa wakati huo wanadamu hawakuwa na amri ya kuiadhimisha siku ya SABATO. Kwao siku zote zilikuwa sawa. Lakini, SABATO kwa wana wa Israeli ilianzia wakati wa Musa. Biblia Takatifu inasema kwamba: "Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, ...lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, ...wala wanyama wako.., ..wala mgeni aliye ndani ya malango yako." (Kutoka 20:8-10) Hapo Mungu anampa Musa amri ya kuikumbuka siku ya Sabato kwa kutokufanya kazi yo yote yeye wala wana wa Israeli wala wageni wo wote walio katika miji yao. Mungu alisema hivyo kwa sababu kuu mbili, nazo ni zifuatazo: (a) Kuiweka siku hiyo kwa ajili ya kumwabudu Mungu badala ya wana wa Israeli kuitumia siku hiyo kwa kazi zao binafsi. (b) Wapumzike kutokana na kazi walizozifanya kwa mfululizo wa siku sita ili wapate nguvu mpya itakayowaongezea ufanisi wa kufanya kazi katika siku sita nyingine zinazofuatia. Hilo ndilo lilikuwa lengo la Mungu kuwaambia wana wa Israeli wawe na siku ya SABATO (PUMZIKO). Tunapozungumzia Sabato ya wana wa Israeli, ni pana sana na inaadhimishwa tofauti kabisa na jinsi ambavyo wanafanya Wasabato wa leo. Kwa wana wa Israeli, siku ya Sabato iliwekwa wakfu kwa ajili ya Mungu, ilikuwa ishara kwamba watu wale waliunganishwa na Mungu kwa njia ya Agano (mapatano). Vile vile Sabato ya wana wa Israeli haikuwa Sabato ya siku tu (yaani kupumzika tu katika kila siku ya saba ya juma), bali wana wa Israeli walikuwa na SABATO YA SIKU (kupumzika siku ya saba ya kila juma,) walikuwa na MWAKA WA SABATO, na pia walikuwa na SABATO YA MASHAMBA. Sabato hizo zote zina sheria zake ambazo walilazimika kuzitekeleza.  Sabato kwa wana wa Israeli ilikuwa ni ifuatavyo: i/: Mtu aliyefanya kazi siku hiyo alihukumiwa kifo. Ni marufuku kabisa kufanya kazi siku ya Sabato. Kulingana na torati, ni marufuku mtu kufanya kazi yo yote katika siku ya Sabato. Endapo mtu ye yote akikiuka agizo hilo, alihukumiwa adhabu ya kifo (aliuawa). Mungu anasema kwamba: "Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; ...Kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa." - (Kutoka 31:14-15) Hayo ndiyo maneno ya Mungu Mwenyewe wala si maneno yangu mimi au ya Musa, bali ni Mungu Mwenyewe. Kwa kila mtu aliyeinajisi Sabato; hapakuwa na majadiliano wala kuomba msamaha, bali hukumu hiyo utolewa hapo hapo. Na pia kwa msisitizo neno la Mungu linasema: "...wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele." - (Kutoka 31:16) Hadi hapo napenda niulize swali. Je! Wasabato wa leo wanawaua watu wote wafanyao kazi yo yote katika siku ya Sabato? Je! Wasabato wa leo wanaua kila mtu anayenajisi siku ya Sabato? Je! Wasabato wa leo wanatii amri ya Mungu au wameshika mafundisho ya nani? Majibu yote tutayafahamu huko mbeleni katika somo hili. Sheria nyingine ya Sabato ni hii ifuatayo: ii/: Wanyama wote wa kufugwa watumikao katika kufanya kazi; mfano farasi, ng'ombe, punda, n.k pia nao walipaswa kupumzika siku ya Sabato. Neno la Mungu linasema kwamba: "...siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako." - (Kutoka 20:10) Kwahiyo si wanyama tu waliopaswa kupumzika kwenye siku ya Sabato, bali pia wote hawa walitakiwa wasifanye kazi: "...wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako." Hivyo ndivyo jinsi sheria ya Sabato ilivyo. Labda niulize swali: Je! Wasabato wa leo wanafanya hivyo?  iii/: Nchi ya mashamba, ilipumzishwa baada ya kulimwa kwa mfululizo wa miaka sita. Ule mwaka wa saba unaitwa mwaka wa Sabato kwa ajili ya mashamba. Neno la Mungu linasema kwamba: "Panda shamba lako miaka sita, ...na kuyachuma matunda yake; lakini katika mwaka wa saba itakuwa ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi, ...usipande shamba lako, wala usipelee shamba lako... Hicho kimeacho chenyewe.., usikivune, ...utakuwa mwaka wa kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi." - (Walawi 25:3-5) Hapo tunaona Mungu anasema "...mwaka wa saba itakuwa ni Sabato ...usipande shamba lako, wala usipelee shamba lako...utakuwa mwaka wa kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi." Niulize swali jingine tena hapa: Je! Wasabato wa leo wanafanya hivyo?  Kama jibu ni "HAWAFANYI HIVYO." Je! Nani amewapa amri ya kupunguza sheria za Mungu kwa kuchagua yale machache wayatakayo alafu wakayaboresha? Je! Huko ni kushika sheria ya Mungu au ni kushika mafundisho ya wanadamu? Sheria nyingine ya Sabato ni hii ifuatayo: iv/: Kuwasamehe wenye madeni wote unao wadai. Hiyo ni amri wala si hiari. Mungu anasema kwamba: "Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio. Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenzake, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya BWANA." - (Kum 15:1-2) Hapo neno "...maachilio..." limetumika kumaanisha "...samehe..." kila deni unalodai kwa ndugu yako au kwa mwenzako ye yote yule. Ndiyo maana hapo Mungu anasema: "...kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenzake, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye..." Mbiu hiyo ya maachilio hupigwa kila mwishoni mwa miaka saba. Hapa napo tena niulize swali: Je! Wasabato wa leo wanafanya hivyo? Na pia, Sheria nyingine ya Sabato ni hii ifuatayo: v/: Makuhani katika mwaka wa Sabato, walipaswa kuwakusanya watu wote kwa ajili ya kuwasomea sheria (Torati) hadharani, ili kuwakumbusha watu wajibu wao kwa Mungu. Masomo yale yalitekelezwa mahali rasmi pa ibada ambapo watu walikusanyika ili washerehekee sikukuu ya Vibanda. Biblia inasema: "Musa akaiandika torati hii, akawapa makuhani, ...na wazee wote wa Israeli. ...akawaamuru, ...Mwisho wa kila mwaka wa saba, wakati wa maachilio, wakati ulioamriwa wa sikukuu ya vibanda, ...Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto, na mgeni ...wapate kusikia na kujifunza, na kumcha BWANA, Mungu wenu, na kuangalia kutenda maneno yote ya torati hii..." - (Kum 31:9-13) Biblia Takatifu inaposema "...WAPATE KUSIKIA NA KUJIFUNZA, ...NA KUANGALIA KUTENDA MANENO YOTE YA TORATI HII..." Maana yake ni kwamba kila kilichomo ndani ya torati ni lazima kukitekeleza pasipo kupunguza neno wala kuongeza neno. Je! Wasabato wa leo wanafanya hivyo? SABATO ni amri inayopatikana ndani ya TORATI. Na pia tunapozungumzia “TORATI” maana yake ni “SHERIA” yote ambayo ndani yake tunakuta kipenyere cha Sabato. Kwa maneno ya sasa tunaweza kuifananisha TORATI na KATIBA alafu SABATO ni IBARA iliyomo ndani ya KATIBA. Biblia inalitumia neno TORATI au SHERIA kwa mtazamo mbali mbali; Upo wakati limetumiwa kwa maana ya amri au maagizo na maelezo ya jumla ambayo yametolewa na Mungu, au na wazazi, serikal, au walimu (Mwa 26:5; Kut 18:20; Zab 119:18-20, 51-61; Mhu 3:1; 6:20), mara nyingine linahusika kutaja Agano la Kale kwa ujumla, na pia mara nyingine linakuwa linataja kwa sehemu ya Agano la Kale tu hususani vile vitabu vitano vya Musa (Mt 5:17; Lk 24:44; Yn1:45; 15:25) ambavyo vilijulikana kwa jina la PENTATUKI. Jina hili "PENTATUKI" linatokana na maneno mawili ya lugha ya Kiyunani (Kigiriki) nayo ni "PENTA" maana yake ni "TANO", na neno "TEUCHOS" maana yake ni "KITABU". Waebrania waliiita PENTATUKI yote SHERIA au TORATI. Vitabu hivyo ni MWANZO (GENESIS), KUTOKA (EXODUS), WALAWI (LEVITICUS), HESABU (NUMBER) na KUMBUKUMBU LA TORATI (DEUTERONOMIUM). Hiyo ndiyo  maana halisi ya TORATI au SHERIA ilivyo ki mtazamo wa Biblia. Kwa hiyo tumeona Biblia inasema: "Musa akaiandika torati hii, akawapa makuhani, ...na wazee wote wa Israeli. ...akawaamuru, ...Mwisho wa kila mwaka wa saba, wakati wa maachilio, wakati ulioamriwa wa sikukuu ya vibanda, ...Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto, na mgeni ...wapate kusikia na kujifunza, na kumcha BWANA, Mungu wenu, na kuangalia kutenda maneno yote ya torati hii..." - (Kum 31:9-13) Torati hiyo ni maagizo na amri zote zilizomo katika vitabu vyote vitano (PENTATUKI); hiyo ndiyo ambayo waliamuriwa kuishika pasipo kuongeza wala kupunguza neno lo lote lile. Pia tunaona Mungu anamwambia Musakwamba: "Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto, na mgeni wako aliyemo malangoni mwako wapate kusikia na kujifunza, na kumcha BWANA, Mungu wenu, na kuangalia kutenda maneno yote ya torati hii." - (Kum 31:12) Maana yake ni kwamba, wote wanalazimika kusikia, kujifunza, kumcha Mungu, na kutenda maneno yote ya hiyo sheria ambayo Musa amepewa na Mungu. Endapo ukiishi kwa kushika torati / sheria ni makosa kabisa kubagua cha kushika kulingana na matakwa yako binafsi; kwa maana imeandikwa: "Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, Amina." - (Kum 27:26); na pia ni makosa kuongeza wala kupunguza neno lo lote lie ambalo Mungu ameamuru lifanywe. Kwa maana Mungu anasema: "Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za BWANA, Mungu wenu, niwaamuruzo." - (Kum 4:2) Hivyo basi, Sabato ni moja kati ya amri za Mungu zilizomo ndani ya TORATI. Pia Sabato ni pana sana na inazo sheria zake kama jinsi tulivyojifunza hapo awali. Kwa maneno ya sasa tunaweza kuifananisha TORATI na KATIBA alafu SABATO ni IBARA iliyomo ndani ya KATIBA. Kwa mara nyingine tena niulize swali; Je, Wasabato wa leo wanatekeleza yote yaliomo ndani ya torati kama jinsi Mungu alivyo amuru? Endapo kama - Hawatekelezi! JE! ASILI YA WASABATO WA LEO NI IPI? Kumbuka Waswahili husema: "Ukweli usioujua hauwezi kukusaidia." Nami pia nasema kwamba: "Uongo usioujua ni vigumu kuuepuka." Lengo kuu la kujifunza ni kuifahamu kweli yote; Lakini zingatia kwamba: "Hauta elewa mpaka pale utakapo funguka akili; na hautafunguka akili mpaka pale utakapoikubali kweli." HISTORIA YA CHIMBUKO LA WASABATO WA LEO. Bila shaka kama umefatilia vizuri somo hili utakuwa unaelewa vizuri maana ya neno SABATO kwa mtazamo wa ki-Biblia. Sasa basi; Wasabato wa leo wanajulikana kwa jina la "Waadventista Wasabato" yaani "Seventh Day Adventists". Tofauti na Wakristo wengine: - Wasabato wa leo (SDA) wao siku yao ya ibada ni siku ya saba ya juma (Jumamosi ya kisasa ambayo kwa mujibu wa Biblia Takatifu ndiyo siku ya saba ya juma yaani SABATO).  - Woa wanazuiwa kula baadhi ya vyakula ambavyo vinaliwa na Wakristo wa madhehebu mengine. (huko mbeleni katika somo hili tutajifunza kuhusu vyakula). IMANI YA WASABATO WA LEO (SDA) ILIANZA KAMA IFUATAVYO: Waasisi (waanzilishi) wa imani hiyo ni: i/: William Miller Alizaliwa mwaka 1782 katika mji wa Pittsfield, Massachusetts, Marekani na alifariki mwaka 1849. Alizaliwa kwenye familia ya Kikristo lakini aliuacha (aliasi imani ya Ukristo) alipokuwa kijana. Hakuiamini Biblia Takatifu kuwa ni Neno la Mungu. Katika mwaka wa 1816 aliongoka na kuurudia Ukristo, akapenda kusoma unabii kwa kina uliohusu kurudi kwa Yesu Kristo. Kutokana na kujifunza kwake unabii, alishawishika kwamba mwisho wa dunia (Kiyama) ingakuwa mwaka wa 1843. Ulipofika mwaka 1831 alitangaza hadharani maono ya unabii aliokuwanao kuhusu mwisho wa dunia. Akapata umahalufu sana sehemu nyingi na hatimaye akawa mhubiri wa dhehebu la KIBAPTISTI. Kutokana na kwamba mwisho wa dunia unaambatana na kurudi kwa Yesu Kristo ambako kwa lugha ya Kiingereza huitwa "Christ's Advent", wafuasi wake walianza kujulikana kama "Adventists" au "Waadventista"; yaani "Watarajiao kurudi kwa Kristo." Ikumbukwe kwamba: William Miller alikuwa ni mhubiri wa dhehebu la KIBAPTIST, na hadi kufa kwake kamwe hakuwahi kuwa muumini wa dhehebu la Waadventista Wasabato (SDA) kwa sababu yeye alifariki hata kabla ya dhehebu hilo kuanzishwa; lakini mafundisho yake yamekuwa nguzo katika uasisi wa dhehebu la Waadventista Wasabato (SDA) kama jinsi tutakavyojifunza huko mbeleni katika somo hili. William Miller alikuwa ni Madventista wala si Msabato. William Miller alishawishika kufundisha kwamba mwisho wa dunia (Kiyama) ingekuwa mwaka 1843 kutokana na jinsi yeye alivyotafsiri andiko la kitabu cha DANIELI 9:24-27. Biblia Takatifu inasema: “Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono na unabii, na kumtia mafuta Yeye aliye mtakatifu. Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu  hata zamani zake Masihi aliye Mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati za taabu. Na baada ya yale majuma sitini na mawili, Masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu; na watu wa mkuu atakayekuja watauangamiza mji, na patakatifu; na mwisho wake utakuwa pamoja na gharika, na hata mwisho ule vita kuwepo; ukiwa umekwisha kusudiwa. Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu.” - (Dan 9:24-27) Unabii huo wa Danieli unahusu majuma sabini yaliyowekwa kwa ajili ya watu wa Mungu, na mwanzo wa majuma hayo ni tangu kujengwa upya kwa mji wa Yerusalemu, hadi kukatiliwa mbali kwa Masihi.

0 comments:

Post a Comment