“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo” Rum 10:17.
Imani inatokana na neno la Kristo au neno la Mungu, mtu akilisikia neno na kulifahamu na kuliamini anakuwa na imani katika neno la Mungu. Ni jambo la msingi na muhimu kuliamini neno, ndio maana Mungu amesema;
"Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita; roho yangu haina furaha naye” Ebr 10:38.
Kuamini neno la Mungu.
Asiyeamini neno la Mungu hampendezi Mungu bali amemwasi, hataingia mbinguni. Wana wa Israel walikufa jangwani kwa sababu hawakuamini maneno ambayo Mungu aliowaambia. “Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka jangwani? Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake (mbinguni), ila wale walioasi?
Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutoamini kwao. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao.
Lakini neno lile lilosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliolisikia” Ebr 3:17-19; 4:2.
Imani na matendo.
Mtu anawezaje kuwa na imani na matendo? Anapoliamini neno na kuishi linavyosema, imani ya mtu huyo ni hai. Imani bila matenda haifai imekufa, bali inakamilishwa na matendo.
“Vivyo hivyo na imani, ispokuwa na matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale. Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa na haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake” Yak 2:17,18,22,24.
Kumtumaini Mungu kwa imani.
Mungu yeye ni mkuu wa yote na ni muumbaji wa yote, anatawala duniani na mbinguni na katika yote. Yeye anaweza yote, na amwaminiye yote yawezekana kwake. Mwanadamu anapaswa kumtumaini na kumkiri katika mambo yote na njia zote naye atamfanikisha. Ili Mungu amfanikishe ni lazima aishi kwa kuyafanya maagizo ya neno lake.
“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako” Mit 3:5,6.
“Umtumaini Bwana ukatende mema (maagizo yake), Ukae katika inchi , upendezwe na uaminifu, Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako.
Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya”Zab37:3-5.
“Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Amebarikiwa mtu yule amtegemeaye Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake” Yer17:5,7.
Kusema kwa imani.
Ili uweze kusema kwa imani na mambo yatokee, yapo mambo ambayo unapaswa kuyafahamu.
1.Umtumaini na kumwamini Mungu, hii ni imani ya Kimungu. Ndio maana Bwana wetu Yesu Kristo alisema “mwaminini Mungu” hili neno lina maana ya kuwa na imani ya Kimungu.“Yesu akajibu, akamwambia, mwaminini Mungu” Mk 11:22.
2. Kuishi sawa swa na neno la Mungu. Imeandikwa, Mungu anafanya kazi na wale wampendao ni wale wanaolishika neno lake.
“Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” Yn 14:23.
“Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani,wale walioitwa kwa kusudi lake” Rum 8:28.
3.
Kudumu katika maombi na wakati mwingine kufunga. Bila hivyo huwezi kufanya mambo ya mamlaka katika Mungu, iwe kuhamisha mlima au kutoa pepo.
“……Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]” Mt 17:20,21.
Katika maandiko haya Yesu anatufundisha yote yawezekana kwa imani kidogo, ikiwa tunaomba na kufunga.
NI MIMI NDUGU YAKO
0 comments:
Post a Comment