Pages

Subscribe:

Monday, 12 October 2015

NGAO YA IMANI

IMANI YA UKRISTO
"Katika nyakati hizi za Agano Jipya, imani ya UKRISTO imejengeka kutoka kwa Yesu Kristo ambaye wafuasi Wake wote amewafanya kuwa WATEULE Wake kwa kuwajaza Roho Mtakatifu ambaye ni mfano wa mafuta waliyokuwa wanapakwa wateule
wa Mungu enzi za nyakati za Agano la Kale."

Waswahili husema kwamba: "Ukweli usioujua hauwezi kukusaidia." Nami pia nasema kwamba: "Uongo usioujua ni vigumu kuuepuka." - na: Mwinjilisti Masanja Sabbi.

Hebu soma kwa makini mafundisho haya ili upate kuifahamu iliyo kweli. Mpenzi msomaji,
bila shaka unayo shauku kubwa sana ya kujua ukweli uliojificha katika imani ya Ukristo kwani ni watu wengi tunawasikia wakijiita na kuitwa wao ni "Wakristo" lakini yawezekana wewe haujui nini hasa maana ya neno "WAKRISTO"; na pia chimbuko na asili ya imani hii.

Bila shaka hapa umefungua ukurasa sahihi kabisa na utarajie kujifunza mengi na kweli tupu. Kabla hatujafika mbali katika kujifunza napenda kukupa taadhali / angalizo hili: Mara nyingi katika kujifunza unaweza ukapokea kitu kilicho kipya kwako na wakati mwingine ujumbe huu ukakuudhi kwa sababu umefichua machukizo yaliyojificha katika imani yako au dhehebu lako. Elewa kwamba; Huduma hii haipo kwa lengo la kuitukana dini au dhehebu fulani, bali dhumuni kuu la huduma hii ni kufundisha jinsi kweli ilivyo pasipo kificho. Napenda nikushauri hivi: Lengo la kujifunza ni kutaka kujua / kuelewa kweli yote. Lakini zingatia kwamba: "Hauta elewa mpaka pale utakapo funguka akili; na hautafunguka akili mpaka pale utakapoikubali kweli." Na sasa unaweza ukachukua kalamu na karatasi, au daftari ili uandike point za muhimu unazojifunza ambazo utakuwa ukijikumbushia yale uliyojifunza pindi upatapo nafasi. Baada ya utangulizi huo; napenda tujifunze kwa kina somo letu linalohusu IMANI YA UKRISTO. Hebu tuanze ifuatavyo: IMANI YA UKRISTO CHIMBUKO NA ASILI YA UKRISTO. UKRISTO unatokana na neno KRISTO. Ni sawa sawa na kusema UTANZANIA unatokana na neno TANZANIA kwa sababu UTANZANIA maana yake ni utamaduni wa ki-Tanzania. Unapotamka neno KRISTO unakuwa umetamka kwa kutumia lugha ya Kiyunani (Kigiriki) lakini chimbuko na asili ya neno hilo ni neno MASIHI ambalo ni la lugha ya Kiebrania. Maneno yote hayo mawili; "KRISTO" na "MASIHI" yote yana maana moja ambayo kwa Kiswahili chepesi tafsiri yake ni Mteule wa Mungu au Mpakwa mafuta wa BWANA Mungu. Imani hii ya UPAKWA MAFUTA (UKRISTO au UMASIHI) inatokana na desturi ya Wayahudi katika nyakati za Agano la Kale hususani pindi miongoni mwao walipokuwa wanateuliwa watu kufanya kazi zifuatazo: i/: KUHANI. Kuhani ni mtu aliyeteuliwa na Mungu kwa ajili ya kufanya huduma ya upatanisho kati ya Mungu na wanadamu. Makuhani walikuwa ni wakuu wa dini ambao kazi yao ni kuwapa watu maagizo ya Mungu au miungu yao (hata wapagani walikuwa na makuhani kwa ajili ya miungu wao. Soma Mwanzo 41:45; 47:22 hao walikuwa makuhani wa Misri)  na pia makuhani walikuwa watoaji wa sadaka / kafara ambazo zimeletwa na watu kwa lengo la shukrari, au upatanisho wa dhambi zao kwa Mungu, au miungu wao. UFAFANUZI - ZINGATIA HILI: Utofauti kati ya "Mungu", na "mungu" - unapoandika kwa kuanza na herufi kubwa "M" yaani "Mungu" unakuwa umemtaja Mungu muumba wa vitu vyote; lakini endapo ukiandika kwa kuanza na herufi ndogo "m" yaani "mungu" hapo unakuwa umetaja "miungu" kwa maana ya watu, mizimu, pepo wachafu, au Shetani. Uwe makini sana utumiapo majina hayo. Pia uonapo katika Biblia Takatifu pameandikwa kwa herufi zote kubwa neno "BWANA" unatakiwa ujue hapo limetumiwa badala ya jina YEHOVA  ambalo ndilo jina Mungu alijitambulisha kwa Musa (Kutoka 6:2,6).  Hivyo basi; Mungu aliamuru makuhani wawekwe wakfu kwa kupakwa mafuta kichwani. Tunaona Mungu anamwagiza Musa kwamba: "Nawe umlete Haruni ndugu yako karibu nami, na wanawe pamoja naye, miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani... nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na kuwatakasa, ili wapate kunitumikia Mimi katika kazi ya ukuhani." - (Kutoka 28:1, 41) Hapo tunaona Mungu anamwambia Musa kwamba: "...watie mafuta..." Musa alichukua mafuta na kuyatia kichwani mwao kwa ishara ya kuwa watu hao wamepewa kibali na Mungu cha kumtumikia kwa huduma ya ukuhani. Watu wengine waliopakwa mafuta kwa ishara ya kupewa kibali na Mungu kwa kazi husika ni hawa: ii/: WAFALME WA ISRAELI. Tunaposoma Biblia Takatifu tunaona pia wafalme wa Israeli nao waliteuliwa kwa kupakwa mafuta matakatifu kichwani mwao. Tukimtazama mfalme Sauli tunaona Biblia inatuambia kuwa yeye ni mpakwa mafuta wa Mungu, yaani: "...masihi wa BWANA..." - (1 Sam 24:10). Wakati mfalme Sauli anawekwa wakfu, Biblia Takatifu inatuambia: "Ndipo Swamweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema,.. Nawe utawamiliki watu wa BWANA... hii itakuwa ishara kwako ya kuwa BWANA amekutia mafuta..." - (1 Sam 10:1) Pia tukija kwa mfalme Daudi tunaona naye pia alipakwa mafuta. Hapa tunaona Mungu anamwambia Samweli mtumishi Wake kwamba Samweli aende akampake Daudi mafuta ili awe mfalme wa Israeli. Tunaona Mungu anamwambia Samweli: "...Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta... na Roho ya BWANA ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile..." - (1 Sam 16:12-13) Vile vile mfalme Sulemani naye alipakwa mafuta kwa ishara ya kuteuliwa na Mungu kuwa mfalme wa Israeli. Biblia Takatifu inasema kwamba: "Na Sadoki, kuhani, akaitwaa ile pembe ya mafuta... akamtia Sulemani mafuta... Na watu wote wakasema, Mfalme Sulemani na aishi!" - (1 Wafalme 1:39) Pia tunamwona Mungu anamwambia nabii Eliya kumpaka mafuta Yehu awe mfalme wa Israeli - (1 Wafalme 19:16). Watu wengine waliokuwa wanapakwa mafuta kwa ishara ya kuteuliwa na kupata kibali kwa Mungu kwa ajili ya kazi maalumu, ni hawa wafuatao: iii/: MANABII. Upo wakati pia manabii nao waliteuliwa na Mungu kwa ishara ya kupakwa mafuta. Biblia Takatifu inatueleza jinsi Mungu alivyomwambia nabii Eliya kwamba: "...Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako." - 1 Wafalme 19:16. Watu hao, yaani makuhani, wafalme wa Israeli, pamoja na manabii walikuwa wanateuliwa kwa kupakwa mafuta ambayo ni ishara ya kupata kibali mbele za Mungu kwa ajili ya kufanya kazi waliyopewa. Vile vile haikuwa tu mtu ye yote anaweza kuwapaka mafuta wateule hao, la hasha! Kazi hiyo ilifanywa na watumishi wa Mungu; nao hao watumishi hawakupaka watu ovyo ovyo bali waliongozwa na Mungu mwenyewe kwa agizo Lake. Mungu ndiye aliyechagua wateule Wake. Hiyo ndiyo chimbuko la imani ya UKRISTO, au UMASIHI, au UPAKWA MAFUTA, au UTEULE. Hadi hapo tunakuwa tumefahamu kwamba UKRISTO haukuanzia katika huduma ya Bwana Yesu kama mtu hapa duniani, bali UKRISTO ulikuwepo hata kabla ya Yesu kuja duniani kama mwanadamu. Katika nyakati za Agano la Kale huo UKRISTO au UMASIHI au UPAKWA MAFUTA au UTEULE ulikuwa wa mtu mmoja mmoja katika jamii ya Waisraeli; lakini, bado tunaona wana wa Israeli walikuwa wanatazamia kuja kwa MASIHI Mkuu yaani KRISTO Mkuu ambaye atawatawala watu wa Mungu, atakuwa kuhani kwa kufanya upatanisho, atakuwa nabii kwa kuyasema yale ayaonayo kwa YEHOVA, na pia MASIHI (yaani MTEULE) huyo atatawala milele - (Zaburi 89:3-4; Isaya 9:2-7; 11:1-5; Yeremia 23:5; Ezekieli 34:23-26; Mika 5:2) na unabii wote huo ulikuja kutimia katika Agono Jipya ambalo linamtaja wazi wazi kuwa Yesu ndiye Masihi Mkuu ambaye Yule walimtazamia atakuja - (Yohana 1:41-42). Yesu ndiye "...Mchungaji mmoja..." - (Ezekieli 34:23), ambaye ni Kuhani Mkuu - (Waebrania 7:26), na pia ndiye Masihi Mkuu - (Dan 9: 25-27). Tukisoma Biblia ya King James hapo andiko la Danieli 9:25 inamtaja Yesu kuwa ni Masihi Mwana wa Mfalme ("...Messiah the Prince...") Sasa basi; katika nyakati hizi za Agano Jipya, imani ya UKRISTO imejengeka kutoka kwa Yesu Kristo ambaye wafuasi Wake wote amewafanya kuwa WATEULE Wake kwa kuwajaza Roho Mtakatifu ambaye ni mfano wa mafuta waliyokuwa wanapakwa wateule wa Mungu enzi za nyakati za Agano la Kale. Watu wote wamwaminio na kumtii Yesu wanaitwa WATEULE (ingekuwa ni nyakati za Agano la Kale basi nao wangemiminiwa mafuta kama ilivyokuwa desturi ya wana wa Israeli; lakini kwa sasa wanajazwa Roho Mtakatifu. Biblia inasema: "Nanyi, mafuta yale yanakaa ndani yenu... mafuta Yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo..." - (1 Yohana 2:27) Pia Yesu amesema: "...Yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote... na mambo yajayo atawapasha habari yake." - (Yohana 16:13) na pia Bwana Yesu amesema: "...Roho wa Kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, na Yeye atakuwa ndani yenu." - (Yohana 14:17). Hapo tunaona Biblia inasema: "...mafuta yale yanakaa ndani yenu..." - (1 Yohana 2:27); na pia tunaona imeandikwa: "...Roho wa Kweli... anakaa kwenu, na Yeye atakuwa ndani yenu." - (Yohana 14:17) Mafuta yale katika enzi za Agano la Kale yalitumika kama ishara tu ya kuteuliwa kwao, kwa maana imeandikwa: "...hii itakuwa ishara kwako ya kuwa BWANA amekutia mafuta..." - (1 Sam 10:1), bali kwa sasa Roho Mtakatifu Ndiye mafuta yakaayo ndani ya Wafuasi wote wa Yesu na kuwaongoza; na ndiyo ishara yetu ya kuteuliwa na Mungu, kwa maana imeandikwa: "...mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si Wake... Kwa maana wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu." - (Warumi 8:9, 14). Sasa je! Ni uthibitisho upi unaotubainishia kuwa Yesu ni Masihi / Kristo? Je! YEHOVA alithibitisha hilo? Biblia Takatifu inasema kwamba: "Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli... Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, Mteule Wangu, msikieni Yeye." - (Luka 9:34,35) Sauti hiyo ilikuwa ni ya YEHOVA aliyenena mbele ya Petro, Yohana na Yakobo kwa wazi kabisa kwamba YESU NDIYE MTEULE WAKE. Kumbuka kwamba; enzi za Agano la Kale, kwa wana wa Izraeli ukisema neno "Mungu" unakuwa umemtaja "YEHOVA". Hivyo ndivyo wao walivyomtambua Mwenyezi Mungu kwa jina YEHOVA - (Mwanzo 6:2; Zaburi 83:18; Isaya 26:4; Yeremia 16:21; Habakuki 3:19) Hivyo sauti hiyo ilikuwa ya YEHOVA ikimthibitisha Yesu: "...ikisema, Huyu ni Mwanangu, Mteule Wangu, msikieni Yeye." - (Luka 9:35) Imani hii ya WAKRISTO wa sasa imejengwa kutoka kwa Yesu mwenyewe ndiyo maana tunaona wafuasi Wake wanaitwa WA-KRISTO kwa maana ya kwamba "Wateule wa Yesu." Wafuasi hao wa Yesu walikuwa WATEULE tangu kabla ya watu wa mataifa kuwaita kwa jina la Wakristo - (Matendo 11:26) Bwana Yesu Mwenyewe anasema kwamba: "Si ninyi mlionichagua Mimi, bali ni Mimi niliyewachagua ninyi..." - (Yohana 15:16) Wanafunzi wa Yesu waliteuliwa na Yesu, walijazwa Roho Mtakatifu na Yesu; hivyo walikuwa WATEULE hata kabla ya hao watu wa Antiokia kuwaita hivyo. Kwa hiyo neno MKRISTO lina maanisha "Mfuasi / Mteule wa Yesu." Ndiyo maana Biblia Takatifu inasema: "Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili Zake Yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru Yake ya ajabu." - (1 Petro 2:9) Kila aliye mfuasi wa Yesu ameteuliwa na Mungu. Anayeteua ni Mungu wala si mwanadamu; ndiyo maana hapo tumeona pameandikwa: "...ninyi ni mzao mteule,.. taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu..." Katika nyakati za Agano la Kale kule kupakwa mafuta kichwani kulikuwa ni ishara tu - (1 Sam 10:1) ya kuteuliwa na Mungu; bali, katika nyakati hizi za Agano Jipya, kumpokea Yesu, kutii kila aliloamuru, na kujazwa Roho Mtakatifu ndiko kunakufanya uwe mteule wa Mungu - (Yohana 1:12-13). UKRISTO ni zaidi ya kupakwa mafuta, bali UKRISTO ni UTEULE. Kama jinsi ilivyokuwa katika enzi za Agano la Kale kwamba Masihi (Makristo / Wapakwa Mafuta) walikuwa ni wale tu ambao waliteuliwa na Mungu bali jamii nyingine yote walibaki kuwa ni watu wa kawaida tu; vivyo hiyo hata sasa Wakristo / Wateule ni wale tu waliompokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao na kujazwa Roho Mtakatifu, hao tu peke yao ndio wateule wa Mungu - (1 Petro 2:9). Hiyo ndiyo asili ya UKRISTO na maana halisi ya imani ya UKRISTO sawa sawa na jinsi neno la Mungu lifundishavyo. Lakini, tukizidi kutazama kwa kina imani ya Ukristo wa sasa tunaona imani hii imegawanyika katika sehemu kuu mbili, ambazo ni: (a) Wakristo wanaosali siku ya saba ya juma (yaani Jumamosi au Saturday ya leo). (b) Wakristo wanaosali siku ya kwanza ya juma (yaani Jumapili au Sunday ya leo). Matabaka hayo mawili pia wanapishana katika mafundisho na mapokeo fulani fulani. Japokuwa wote wanajiita Wakristo lakini cha ajabu hawaelewani katika mafundisho yao. Waswahili husema kwamba: "Ukweli usioujua hauwezi kukusaidia." Nami pia nakwambia kwamba: "Uongo usioujua ni vigumu kuuepuka." Je, kati ya makundi hayo mawili ya imani ya Ukristo wa sasa, ni kundi lipi linalofundisha mafundisho ya kweli sawa sawa na jinsi Yesu alivyoamuru? Yesu amesema: "...enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi... na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi..." - (Mathayo 28:18-20) Sasa, je! Ni kundi lipi kati ya hayo mawili linafundisha mafundisho ya uongo? Kabla ya kufufika mbali katika uchambuzi huo wa kuibainisha kweli, napenda nikuulize maswali haya: Je! Unapenda kujifunza? Je! Unapenda kuifahamu kweli? Kama jibu lako ni "NDIYO" sasa basi weka kando ushabiki wa dini au dhehebu. Pia zingatia kwamba: "Hauta elewa mpaka pale utakapo funguka akili; na hautafunguka akili mpaka pale utakapoikubali kweli." Katika utafiti wangu na kujifunza kwangu neno la Mungu nikiwa na watu mbalimbali, nimegundua watu wengi wanachanganywa na majina SIKU (DAYS) zilizopo kwenye juma (wiki). Ninapenda kwanza kuliweka sawa jambo hili ndipo tuendelee kujifunza kuhusu imani ya Ukristo wa sasa. Hebu kuwa makini zaidi ili uweze kuelewa vizuri. Tunapozungumza kuhusu “siku”, katika “juma moja” (wiki moja) kuna idadi ya “siku saba”. Siku hizo zimegawanyika katika matabaka makuu “mitatu”. Naomba uwe makini ili uelewe vizuri. Matabaka hayo ndiyo yafuatavyo: i/: KIBIBLIA. ii/: KIPAGANI, na iii/: KIISLAMU. Inawezekana hapa ukajiuliza: Hapo unamaanisha nini? Usihofu, fatilia kwa makini nawe utanielewa vizuri. Tukianza na siku ya JUMATATU: Kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, kwao siku ya “Jumatatu” ya leo kwao ndiyo “siku ya tatu ya juma”. Tukilivunja vunja neno “JUMATATU” tunapata maneno mawili ambayo ni “JUMA”, na neno “TATU”. Neno “JUMA” maana yake ni “WIKI” au “muunganiko wa siku saba”, na TATU maana yake ni TATU (au THIRD - kwa Kiingereza) Kwa hiyo neno “Jumatatu” maana yake ni “siku ya tatu ya juma (wiki). Mpangilio huu umetokana na desturi ya Imani ya Kiislamu. Tukija KIBIBLIA, siku ya “Jumatatu” ya ki-sasa ni SIKU YA PILI YA JUMA. Ambayo siku hiyo kwa upande wa  WAPAGANI waanaiita MONDAY. Hao WAPAGANI siku hiyo kwao ni kwaajili ya kuabudu MWEZI (moon - kwa Kiingereza). Katika nchi za Ulaya na Asia yapo mataifa yaliyokuwa yakiabudu MWEZI (MOON). Neno MONDAY ni kifupisho cha neno MOON - DAY (Siku ya Mwezi) kwa ajili ya kumuabudu mungu wao mwezi. Tukiingia siku ya JUMANNE: Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, kwao JUMANNE ni SIKU YA NNE YA JUMA. Hiyo ni kutokana na desturi ya imani ya Kiislamu. Lakini tukija KIBIBLIA; siku ya JUMANNE ni siku ya TATU katika JUMA. Lakini kwa WAPAGANI wao siku ya JUMANNE wanaiita “TUESDAY”, ni siku maalumu waliyokuwa wakimuabudu mungu wao aliyejulikana kwa jina la “TIWI”. Siku hiyo wakaiita “Tiw's Day” ambayo baadae ikabadilishwa na kuitwa “TUE 's - DAY” (Siku ya Tue / Tiwi) sawa sawa na jinsi ijulikanavyo leo. Tukiingia kwenye siku ya JUMATANO: Kwa mujibu wa imani ya Kiislamu, wao siku ya JUMATANO ni siku ya TANO katika JUMA (week - kwa Kiingereza). Kwa mujibu wa Biblia Takatifu, siku ya JUMATANO ni siku ya NNE katika JUMA (week - kwa Kiingereza). Lakini kwa WAPAGANI, siku ya JUMATANO wanaiita WEDNESDAY. Siku hiyo kwa Wapagani ni maalumu kwa kumwabudu mungu wao ajulikanae kwa jina la “WEDNE” au “WODEN” ndiyo maana siku hiyo wakaipa jina la “WEDNE 's - DAY” au kwa English nyepesi ni “Wedne ' s Day” (Siku ya Wedne) sawa sawa na jinsi ijulikanavyo leo hata nyakati za leo. Tukiingia kwenye siku ya ALHAMISI: Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, siku ya ALHAMISI ni siku ya SITA katika JUMA (week - kwa Kiingereza). Lakini kwa mujibu wa Biblia Takatifu, siku ya ALHAMISI ni siku ya TANO katika JUMA. Wakati huo kwa upande wa WAPAGANI, wao siku ya ALHAMISI wanaiita “THURSDAY”. Katika siku hiyo hiyo wapo WAPAGANI wanaoabudu “SAYARI YA JUPITER”, na WAPAGANI wengine ni siku maalumu kwao ya kumwabudu mungu wao aitwaye “THOR” au "THUR". Ndiyo maana siku hiyo wakaiita “THUR 's - DAY” au kwa English nyepesi ni “Thur 's Day” (Siku ya Thur). Tukiingia kwenye siku ya IJUMAA: Kwa mujibu wa imani ya Kiislamu, siku ya IJUMAA kwao ni siku ya SABA katika JUMA (week - kwa Kiingereza). Neno IJUMAA ni neno lenye asili ya lugha ya Kiarabu likiwa na maana ya KUSANYIKO (kwa lugha ya Kiswahili). Ndiyo maana katika siku hiyo waumini ya imani ya Kiislamu hukusanyika kwenda kulitaja jina la mola wao (Allah) na kisha baada ya swala (ibada) hutawanyika kwenda kutafuta riziki zao kama jinsi kitabu cha Qur'an kinavyo waamuru. Kwao si siku ya PUMZIKO bali ni siku ya KUSANYIKO. Kwa upande wa Biblia Takatifu, siku ya IJUMAA ni siku ya SITA katika JUMA (week - kwa Kiingereza) Lakini kwa WAPAGANI wao wanaiita FRIDAY. Kwao ni siku maalumu kwa kumwabudu mungu wao aitwaye “FRIGG” au “FREIA”. Ndiyo maana siku hiyo wakaiita FRI -DAY (Siku ya Fri). Tukiingia kwenye siku ya JUMAMOSI: Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, siku ya JUMAMOSI ni siku ya KANZA katika JUMA (week - kwa Kiingereza). Neno “MOSI” maana yake ni “MOJA au KWANZA” (FIRST - kwa Kiingereza). Tumejifunza JUMA moja lina idadi ya SIKU SABA ndani yake; ndiyo maana kwa Waislamu siku ya IJUMAA tumeona ni SIKU ya SABA kwao, alafu JUMAMOSI ni SIKU ya KWANZA kwao. Hapa tunabaini kuwa hizo siku tunazozitumia Waswahili zimetokana na desturi ya mafundisho ya imani ya Kiislamu. Bila shaka hadi hapa tupo pamoja. Tukija upande wa Biblia Takatifu; siku ya JUMAMOSI ni siku ya SABA katika JUMA. Hapa ndipo tunawapata Wakristo wenye imani ya USABATO, wao siku hiyo ni SIKU YA SABATO (PUMZIKO) kwao. Wao hupumzika siku nzima bila kufanya kazi yo yote kwa kuwa ni marufuku kwao kufanya kazi katika siku hiyo. Wasabato hiyo ni siku maalumu kwa ibada tu. Bali Wakristo wasio na imani ya Kisabato wao huendelea na kazi zao kama kawaida. Tukija upande wa WAPAGANI, wao siku ya JUMAMOSI wameipa jina la SATURDAY. Kwao WAPAGANI ni siku maalumu ya kuabudu sayari ya SATURN. Wapo wapagani waliokuwa wanaabudu sayari ya “SATURN” ndiyo maana siku hiyo wakaipa jina la “SATUR - DAY” (yaani Siku ya Saturn). Tukimalizia siku ya JUMAPILI: Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu siku ya JUMAPILI kwao ni siku ya PILI katika JUMA. Lakini kwa mujibu wa Biblia Takatifu; siku ya JUMAPILI ni SIKU YA KWANZA YA JUMA. Je! Tunalitambuaje hili? Biblia Takatifu inasema: "Hata Sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma... Yesu aliyesulibiwa... Amefufuka katika wafu..." - (Mathayo 28:1,5,7) Ndiyo maana wapo Wakristo wanaofanya ibada katika siku hiyo ya kwanza ya juma. Tukiingia kwenye upande wa WAPAGANI siku ya JUMAPILI wao wameipa jina la “SUNDAY” yaani ni “SIKU ya JUA” (SUN). Wapo wapagani ambao wanaabudu JUA. Ndiyo maana siku hiyo wakaiita “SUN - DAY”. Mpendwa msomaji; je! Umewahi kujiuliza kwa nini ndani ya Biblia Takatifu hakuna neno Jumatatu (Monday), Jumanne (Tuesday), Jumatano (Wednesday), Alhamisi (Thursday), Ijumaa (Friday), Jumamosi (Saturday), wala Jumapili (Sunday)? Bali utaona kwenye Biblia Takatifu pameandikwa Siku ya Kwanza, Siku ya Pili, Siku ya Tatu… Siku ya Saba? - (Mwa 1:5,8,13,19,23,31; Mathayo 28:1). Bila shaka ufafanuzi nimeshautoa hapo juu. Hadi kufikia hapo itakuwa imeeleweka vizuri kuhusu SIKU NA MAJINA YAKE. Sasa basi napenda moja kwa moja tujifunze kwa undani kuhusu mgawanyiko huu uliopo katika watu wa imani ya UKRISTO wa leo kwa kuanzia na WAKRISTO WENYE IMANI YA SABATO, kisha tutajifunza kuhusu WAKRISTO WANAOSALI SIKU YA KWANZA YA JUMA.

0 comments:

Post a Comment